Baltazar Mashaka, Mwanza
Samia Suluhu Hassan |
MAKAMU wa Rais, Samia
Suluhu Hassan, amewaagiza wakazi wa Wilaya ya Misungwi kujenga shule za
sekondari na mabweni mengi ya wasichana ili kuwanusuru wasiharibikiwe njiani na
kukatishwa masomo yao.
Alisema mabweni
hayo yakijengwa kwa wingi yatawaondolea wasichana shida na changamoto
mbalimbali wanazokumbana nazo njiani wakati wa kwenda shule na kurudi nyumbani.
Makamu huyo wa rais
pia aliwashukuru na kuwapongeza wananchi wa jimbo la Misungwi kwa kuwapigia
kura yeye na Rais John Magufuli kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
“Nawashukuru kwa
kazi kubwa mliyoifanya na kutuweka ofisini ili tuwatumikie na kwa imani
mliyotuonyesha. Rais pamoja na mimi tuliwaahidi na yote tuliyowaahidi tutayafanya.
Hazitakuwa ahadi hewa na hata mradi huu ninaoufungua ni moja ya ahadi hizo.Zote
zitafanyiwa kazi katika miaka mitano,” alisema
Katika hatua
nyingine, Mama Samia aliwaomba wananchi wa wilaya hiyo kuungana na serikali
kupiga vita rushwa, upotevu wa mapato ya serikali na kufichua uovu kwenye
maeneo yao ili maendeleo yapatikane.
Alisema hayo
katika mkutano wa hadhara, baada ya kuzindua bweni la wasichana wa Shule ya
Sekondari Idetemya lililojengwa chini ya Mradi wa African Assistance Project
(ASAP) kwa gharama ya sh 472,805,000.
Alieleza kuwa
takwimu zinaonyesha kuwa wanawake katika wilaya ya Misungwi ni 177,000 huku
wanaume wakiwa ni 173,000 na kwa takwimu hizo ni wazi maendeleo na uchumi wa
wilaya hiyo unabebwa na wanawake.
Makamu huyo wa
Rais alieleza kuwa kuwekeza kwa kujenga mabweni hayo kutasaidia kukuza taifa
letu kwani wanafunzi hao wataweza kusomea fani mbalimbali za uhandisi, udaktari
na uuguzi na hivyo akaagiza zijengwe shule kama hiyo na kama zipo wajenge
mabweni ya wasichana ili wasiharibikie wala kukatishwa njiani wapate elimu yao.
Pia aliwataka
wananchi pamoja na halmashauri wawe tayari kuchangia fedha ili ASAP waweze
kujenga mabweni mengine na kwamba wasichana hao wanapata huduma ya chakula
shuleni hapo kinachotolewa na mhisani.
“Ningependa
kuona mhisani akiondoka msishindwe kuiendesha shule hii. Wazazi tujipange
vizuri ili mradi uendelee na ndio maana tunahimiza kujitegemea na sisi serikali
kuu tumeanza na ninyi chini muanze sasa.Ingawa tunasaidiwa, tunapokea misaada
pale inapotokea,” alisema.
Akiwa wilayani
Kwimba aliweka jiwe la msingi la bweni la wasichana katika shule ya Sekondari
ya Askofu Mayala Girls na kisha kupanda miti ambapo aliahidi kuchangia ujenzi
wa kituo cha afya Ibindo mifuko 200 ,mifuko 100 itatoka katika ofisi yake na
mingine kwa mkuu wa mkoa wa Mwanza, mabati 200 kai ya hayo 100 yatatolewa na
Mbunge wa Jimbo la Sumve, Richard Ndassa.
Aidha,Mbunge wa
Jimbo la Misungwi Charles Kitwanga “ Mawema matatu” alimweleza Makamu wa Rais
huyo kuwa wananchi wa jimbo hilo wamejipanga na wako kwenye mkakati wa kujenga
shule ya sekondari ya wasichana wenye vipaji maalum wanaofanya vizuri kwenye
masomo yao ambayo itakuwa na kidato cha kwanza hadi cha sita itakayoitwa Eme
Emilembe.
Awali Mkuu wa
Mkoa wa Mwanza John Mongella akimkaribidha Makamu wa Rais alisema wananchi wa
Misungwi wameonyesha kwa vitendo kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano ya
Hapa Kazi Tu kwani hosteli hiyo ya mfano wataitumia na kuisimamia ili mabweni
ya aina hiyo yajengwe katika wilaya za mkoa huo.
Samia baada ya
kuzindua mradi huo wa mabweni ambao ni wa kisasa ukiwa na mambo muhimu ya
chakula na malazi aliendelea na ziara yake wilayani Kwimba ambapo alizuru
katika shule ya Sekondari ya Mayala Girls kabla ya kuelekea Magu kuendelea na
ziara hiyo
0 comments:
Post a Comment