Suleiman Msuya
MIEZI sita tangu watu wanane wauawe kwa
kuchinjwa katika eneo la Kibatini, Mtaa wa Mlemi, Kata ya Kibatini mkoani Tanga,
wakazi wa eneo hilo wameanza kurejea kwa kusuasua, huku hofu juu ya usalama wao
ikiendelea kutanda.
Mbali na hali hiyo, ujenzi wa nyumba za wajane
wa wanaume waliouawa kwenye tukio hilo umekamilika kwa asilimia 97.
Hayo yalielezwa na Mwenyekiti wa Mtaa wa
Mlemi, Shaban Muumin alipokuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na
mwandishi wa habari hii kutoka Tanga.
Mwenyekiti huyo alisema wakazi waliokuwa
wakiishi Kibatini hawana amani na eneo
hilo, licha ya kuwa na ulinzi hivyo wanaendelea kuwaelimisha ili wanaotaka
warejee.
“Tangu tukio la mauaji ya watu wanane la
Mei 30 pale Kibatini wakazi wamekuwa wakisuasua kurejea kwenye makazi yao na familia
ambazo wanaume waliuawa zimehamia Kiomoni,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa kwa sasa
hali ya Kibatini na Amboni zina utulivu, lakini wananchi bado wana hofu inayosababisha
washindwe kurejea kwenye makazi yao.
Alisema inawezekana kusuasua kurejea
katika makazi yao kunahusiana na ukweli kuwa tangu tukio litokee hawajapata
taarifa rasmi ya wahusika ni nani.
Akizungumzia ujenzi wa nyumba za wajane
ambazo ni ahadi ya wabunge wa Mkoa wa Tanga, Meya wa Jiji la Tanga, Selebosi
Mustapha alisema hadi jana umekamilika kwa asilimia 97 na kilichobaki ni
milango tu.
“Kimsingi sikuahidi kujenga nyumba ila
kwa nafasi yangu ya umeya nimefuatilia na wakati mwingine wahusika wanakuja
kwangu kufuatilia baadhi ya mahitaji na ninawaekeleza nini cha kufanya,”
alisema.
Mustapha alisema katika tukio hilo
aliahidi kumsomesha chuo cha ufundi mtoto ambaye alishuhudia baba yake
akichinjwa na ameanza kuitekeleza.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Wilaya ya Tanga, Lucia Mweru ambaye ni mbunge wa viti maalumu na msimamizi wa
utekelezaji wa ujenzi huo, alisema kilichobakia ni milango ambayo Mbunge wa
Viti Maalumu mkoani hapo, Ummy Mwalimu ameahidi kuitoa siku yoyote.
Mweru aliwataka wahusika kuwa na subira
kwani kila kitu kinaenda kama kilivyopangwa na hakuna kitakachowakwamisha.
“Kwa sasa tunashughulikia milango
ikikamilika nadhani itapelekwa kwani Mbunge Mwalimu anaishughulikia,” alisema.
Alisema nyumba hizo tatu zimejengwa kwa
miti na matope na kupauliwa kwa bati na kwamba kila moja inagharimu zaidi ya
sh. milioni 3.
Tukio hilo la kinyama lilitokea Mei 30
mwaka huu majira ya saa saba usiku ambapo watu wanane walichinjwa kama kuku na
watu wanaosadikiwa kuwa ni magaidi wanaojificha katika mapango ya Amboni.
Waliochinjwa ni Issa Hussein (50), Mkola
Hussein (40), Hamis Issa (20) wote wa familia moja, Mikidadi Hassan (70),
Mahmood (40), Issa Ramadhan (25 na Kassim.
Issa aliacha mke Mwanaisha Amir na
watoto saba ambao ni Hussein, Juma, Amir, Fatuma, Rashid na Ashura ambapo mmoja
anasoma Sekondari na watatu shule ya msingi.
Mjane Aisha Said alibainisha kuwa
ameachwa na watoto sita ambao ni Abuu, Hessein, Salimu, Ali, Ramadhan na Said.
0 comments:
Post a Comment