Sharifa Marira
SERIKALI imesema haijashindwa kudhibiti ‘Panya Road’ bali vikundi hivyo
hutekeleza uhalifu kwa kuvizia kutokana na ukweli kwamba askari Polisi hawako
kila mtaa.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu
Nchemba wakati akijibu hoja za wajumbe wa kundi la mtandao la WhatsApp
linalojulikana kama Tanzania Yetu 2016 ambao waliomba asikilize hoja zao na
kuzipa majibu kama waziri kwa kuwa naye ni mjumbe wa kundi hilo na kueleza kuwa
Serikali imejipanga kuwakamata ‘Panya Road’ wote.
Baadhi ya wajumbe walieleza kwamba ‘Panya Road’ wanasumbua maeneo mengi
nchini wakihoji iwapo Jeshi la Polisi limeshindwa kufanya kazi yake.
Hata hivyo, Mwigulu katika majibu yake alisema: “Jeshi letu
halijashindwa kukabiliana na ‘Panya Road’, ingekuwa hivyo hali ingekuwa mbaya
sana, ila wanafanya kuvizia kwa kuwa askari hawako kila mtaa.”
Aliongeza: “Kwa sasa tutakamata wote, wanapaswa kujua kuwa watakutana na
mkono wa sheria wananchi wasijali Jeshi letu liko imara hawatasumbuliwa na
kundi hili.”
Kuhusu kurundikana kwa mahabusu, Mwigulu alisema hiyo ni changamoto nyingine ambayo
wanaiangalia namna ya kufanya, lakini
pia njia ya kutojaza mahabusu wasio wa lazima kutokana na makosa itazingatiwa,
wenye kesi kubwa sawa wabaki, lakini wengine si lazima, kwa kuwa hawawezi
kutoroka.
Suala lingine lililoibua mjadala ni kuhusu polisi kuchelewa kufika
maeneo ya matukio ambapo waziri alisema: “Kuna tatizo la usafiri, tunalifanyia
kazi yapo maeneo wanakosa mafuta, mazingira haya ndiyo nayafanyia kazi, maeneo
mengi mpaka wanathubutu kumwambia mwenye tatizo awape mafuta ili wakamkamatie
mtuhumiwa, Serikali inalifanyia kazi hili.”
Waziri aliombwa pia aeleze chanzo cha ajali kwa anavyojua yeye, ambapo
alijibu kuwa ajali zinasababishwa na mambo mawili kwa kiasi kikubwa; uzembe wa
madereva na uchakavu wa vyombo, madereva wanakwenda kasi kupindukia na vyombo
vyao havijafanyiwa ukarabati.
Mmoja wa wajumbe alimwomba Mwigulu kuhakikisha kuwa katika kipindi
chake, polisi wanafahamu umuhimu wa kukamata watu bila kuwapiga na
kuwadhalilisha, ambapo alikubaliana nalo hilo, lakini akahadharisha kuwa
kukabiliana na majambazi lazima ubabe pia utumike, hivyo kuwaagiza askari
wapambane nao kwa nguvu zote.
0 comments:
Post a Comment