Hussein Ndubikile
Profesa Joyce Ndalichako |
WALIMU nchini wametakiwa kutoa adhabu ya
viboko kwa kuzingatia waraka na maelekezo ya Serikali ya jinsi ya utoaji adhabu
hiyo hususan kwa makosa makubwa yakiwamo ya wizi, uvutaji bangi, kupigana na
kuharibu mali za shule.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam juzi na
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako kwenye
ufunguzi wa mdahalo wa kujenga na kukuza maadili, haki za binadamu,
uwajibikaji, utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa.
Alisema kwa mujibu wa waraka huo, walimu
na viongozi wa shule wanatakiwa kuweka bayana makosa na hatua za kinidhamu
zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya wanafunzi wanaobainika kuvunja sheria.
“Naomba nichukue fursa hii kuielewesha
jamii, kuwa sheria hizi zimetungwa kuadabisha wanafunzi ili wawe kwenye mstari
sahihi utakaowasaidia kujifunza si vinginevyo,” alisema.
Alisema ili kuhakikisha hilo
linafanikiwa, wazazi na walimu wanatakiwa kushirikiana kutimiza azma
iliyokusudiwa ya kumpa mwanafunzi elimu na stadi bora itayojenga misingi ya
maadili inayokubalika kwenye jamii.
Alisisitiza kuwa Serikali imebaini
kuwapo malalamiko kwa baadhi ya walimu na bodi za shule zimekuwa zikipelekewa
wanafunzi wakorofi na zinawatetea bila
kuchukua hatua stahiki hali inayowapa kiburi na kuamua kuwafanyia vitendo
viovu.
Aliagiza kuacha kuingiza siasa kwenye
usimamizi wa maadili huku akitaka wahusika kuzingatia sheria, kanuni, taratibu
na maelekezo yanayotolewa.
Aliasa wanafunzi kuepuka kuwa wahanga wa
teknolojia inayochochea kwa kiasi kikubwa chanzo cha kuwabadili mienendo na
misingi ya maadili yakiwamo matumizi ya mitandao ya kijamii.
Pia aliwaasa kuacha kuangalia masuala
yasiyofaa kwenye mitandao hiyo badala yake waitumie kujifunzia masomo yao.
0 comments:
Post a Comment