Claudia Kayombo
Dk. Egid Mubofu |
KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania
(TBS), Dk. Egid Mubofu, ametoa wito kwa jumuia za wafanyabiasha wenye viwanda
kuzingatia viwango ili kujipatia uhakika wa soko la ndani na nje ya nchi
wanapozalisha bidhaa zao.
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa
Uandaaji wa Viwango wa shirika hilo, Edna Ndumbaro wakati wa maadhimisho ya
Siku ya Viwango Duniani, iliyofanyika kitaifa makao makuu ya shirika hilo Dar
es Salaam, Dk. Mubofu alisema ni vema wajasiriamali wadogo na wa kati
wakaitumia TBS kukuza ubora wa bidhaa.
“Mojawapo ya sababu zinazozifanya bidhaa za nchi
zinazoendelea ikiwemo Tanzania kushindwa kupenya na kuingia katika masoko ya
kimataifa ni kushindwa kukidhi matakwa ya viwango.
“Lakini pia wakati mwingine bidhaa hizo hushindwa kuingia
katika soko la kimataifa au la kikanda kutokana na tofauti katika matakwa ya
kiwango cha bidhaa husika baina ya nchi na nchi,” alisema Dk. Mubofu.
Aliongeza kuwa shirika hilo linapozidi kusonga mbele,
linashirikana na taasisi za kimataifa za viwango kusaidia katika maendeleo ya
teknolojia mpya ambazo zitachochea maendeleo ya uchumi na hivyo kuchangia
katika ustawi wa Watanzania wote.
Dk. Mubofu alitanabaisha kuwa bidhaa nyingi zinahitaji kufanyiwa
vipimo na kutakiwa kukidhi matakwa ya kiwango husika kabla ya kupelekwa sokoni.
Katika biashara zinazohusisha nchi na nchi au mabara,
chombo huru kisichoegemea upande wowote kinahitajika ili kukagua mtiririko wa
uzalishaji, kufanya vipimo na kuthibitisha ubora wa bidhaa au huduma husika.
0 comments:
Post a Comment