Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Andrew Mkapa
|
WAKALA wa
Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) umetoa wito kwa vijana nchini kutumia
fursa mbalimbali za mafunzo ya ujasiriamali na biashara ili kujijengea uwezo wa
kujiamini wanapoamua kujiingiza katika biashara.
Naibu Msajili wa
Wakala (Sheria za Biashara), Andrew Mkapa, amesema kuwa mafunzo ya ujasiriamali
na biashara ni nguzo muhimu kwa vijana, hasa wanapokuwa na malengo ya kujiajiri
kwani mafunzo hayo hutoa mwongozo.
“Nawashauri vijana
kujitokeza kwenye mafunzo ya ujasiriamali na biashara ili muweze kujijengea
uwezo na kujua umuhimu wa kurasimisha biashara zenu ili mtambulike na mamlaka
husika,” alisema
Mkapa alitoa
wito huo mwishoni mwa wiki, baada ya kutoa mada kwenye semina ya ujasiriamali
kwa vijana iliyoandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi kwa lengo la
kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri.
Mkapa aliwataka
vijana kuondokana na dhana ya kusubiri kuajiliwa pindi wanapomaliza shule badala
yake wajikite zaidi kwenye kujiajiri wenyewe kwenye biashara na shughuli
nyingine za kijamii.
“BRELA imeamua
kujikita zaidi katika kutoa elimu ya mafunzo ya kurasimisha biashara kwa vijana
ili kuwahamasisha wapate ufahamu wa namna ya kuanzisha kampuni na majina ya
biashara ili waweze kutambulika kisheria,” alisisitiza.
Mkapa ambaye pia
alitoa mada iliyowasisimua zaidi vijana, alimpongeza DC Hapi kwa jitihada za
kuwakutanisha vijana pamoja na kutoa mafuzo ya ujasiriamali na biashara.
“Kwa niaba ya
Ofisa Mtendaji Mkuu na Msajili wa Kampuni, nachukua fursa kumpongeza mkuu wa
wilaya, wawezeshaji na washiriki wote kwenye mafunzo haya,” alisema na kuongeza
kuwa Brela ipo tayari muda wote kutoa elimu jinsi ya ya kusajili makampuni,
jinsi ya kusajili majina ya biashara na faida zake.
Haya mafunzo
yana maana na yatawasaidia sana vijana pindi watakapoanza kuunganishwa na fursa
mbalimbali zinazotolewa kama vile ya mikopo kwani tayari watakuwa na uwelewa
mkubwa wa kuzitumia fursa.
“sio tu kwa
vijana hawa waliohudhuria leo hapa lakini ni kwa watu wote kwa ujumla nchi
nzima ni muhimu katika karne hii ya sasa kufanya biashara zilizo rasmi,”
alisisitiza Mkapa
Mshiriki wa
mafunzo, Bw. Medson Moshi ni miongoni mwa vijana waliohudhuria semina hiyo
na aliwataka na kuwahimiza vijana wengine kuchangamkia fursa kama hizo na
kuachana na mtazamo wa kusubiri kulipwa fedha ili kuweza kudhuria semina za
mafunzo kama hiyo.
0 comments:
Post a Comment