*Wapewa muda hadi Januari kukamilisha
*Vinginevyo watakuwa wameshindwa kasi
Mwandishi Wetu
WAKUU wa mikoa saba wamo hatarini ‘kutumbuliwa’ kutokana
na kushindwa kutimiza agizo la Rais John Magufuli la kukamilisha utengenezaji
madawati kwa wakati.
Akiitaja mikoa hiyo, wakati akipokea madawati 3,500
yaliyotolewa na benki ya NMB, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George
Simbachawene alisema mikoa hiyo ni Geita ambao unadaiwa madawati 83,975 (68,306
kwa shule za msingi, na sekondari ni 15,669).
Mikoa mingine ni Mara unaodaiwa madawati 15,843 kwa shule
za msingi, wakati za sekondari ni 1,135; Dodoma (msingi ni 10,592, sekondari
4,281), Rukwa (msingi 9,634, sekondari 1,340) na Simiyu (msingi ni 10,209 na
sekondari ni 647).
Wakati mikoa hiyo ikidaiwa madawati kwa shule za msingi
na sekondari, mikoa mingine inayodaiwa madawati kwa ajili ya shule za msingi
pekee ni Mwanza (41,438) na Kigoma ambao wanadaiwa madawati 31,171.
“Leo (jana) ninapokea madawati haya 3,500 kutoka NMB
ikiwa ni mpango mkakati wao wa kusaidia kutatua upungufu wa madawati nchini,
huku kukiwa na mikoa hiyo ambayo bado haijakamilisha. Ninatoa hadi Januari mwakani
wawe tayari wamekamilisha.
“Endapo watakuwa wameshindwa kukamilisha hadi muda huo,
itakuwa wameshindwa kuendana na kasi itakiwayo. Lakini naamini kuwa
watakamilisha na ninatarajia kuwa kila mhusika atasimamia ipasavyo ukamilishaji
huo,” alisema Simbachawene.
Akizungumzia madawati hayo ya NMB, Simbachawene alisema
kwa namna ya pekee, Serikali inaishukuru benki hiyo kwani imekuwa mstari wa
mbele kuchangia madawati ikiwa ni mpango mkakati wao wa kutatua changamoto
hiyo.
“Kwa niaba ya Serikali, naishukuru NMB kwani imekuwa
mstari wa mbele kuisaidia Serikali kuondokana na upungufu wa madawati nchini.
Kupitia mpango wao wa CSR, benki iliahidi kutoa Sh bilioni 1.5 kwa ajili ya
madawati na ndiyo kama haya ninayopokea,” alisema Simbachawene.
Mtendaji Mkuu wa NMB, Ineke Bussemaker alisema utoaji wa
madawati hayo ni utimizaji ahadi yao kwa Serikali ya kuchangia madawati yenye
thamani ya Sh bilioni 1.5.
“Kupitia mpango wetu wa CSR, tulilenga kutoa madawati
yenye thamani ya Sh bilioni 1.5 na kwa mwaka huu, tumeshatoa madawati 10,000
yenye thamani ya Sh milioni 900. Madawati mengine yenye thamani ya sh milioni
600 itatolewa mapema mwakani,” alisema Bussemaker.
0 comments:
Post a Comment