Salha Mohamed
Baraka Mashauri |
TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya
Fahamu (MOI) imeshindwa kutoa matibabu kwa kijana Baraka Mashauri (35) mwenye
urefu wa futi saba anayesumbuliwa na nyonga.
Kijana huyo ni wa kwanza kupokewa akiwa
na urefu zaidi, alifika hospitalini hapo mwishoni mwa Oktoba kutokana na
matatizo ya nyonga kwenye mguu wa kushoto kutokana na kuanguka.
Akizungumza na JAMBO LEO jana Dar es
Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma, Jumaa Almasi alisema kijana
huyo anaishi Musoma Vijijini eneo la Majita ‘B’.
“Ni mrefu sana ukilinganisha na Mtanzania
wa kawaida, kwani ana futi saba, alipokuwa akitibiwa alitakiwa kufanyiwa
upasuaji wa nyonga,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo alitakiwa
kufanyiwa kipimo cha X-ray lakini imeshindikana baada ya madaktari kumfanyia na
kutopata majibu kama walivyotarajia ili kufanikisha upasuaji.
Alisema hata vitanda vinavyotumika
kuweka wagonjwa kwa ajili ya upasuaji hakimtoshi kulala kwani ana urefu wa futi
saba huku kitanda kikiwa na urefu wa futi sita.
“Hata vifaa tulivyokuwa tukitumia
kumfanyia vipimo havikukaa sawasawa sababu ana mfupa mkubwa sana wa nyonga,
mashine zimeshindwa,” alisema.
Almasi alifafanua, kuwa kutokana na hali
hiyo, kijana huyo anatakiwa kuagiziwa chuma maalumu kutoka kiwandani kwa oda
maalumu ili kitengenezwe au akafanyiwe upasuaji huo nje ya nchi kulingana na
maumbile yake.
Aliongeza kuwa bado taasisi hiyo
inafanya juhudi za kuwasiliana na taasisi nyingine nje ya nchi, ili kutoa
huduma kwa kijana huyo.
0 comments:
Post a Comment