Mary Mtuka
KAMPUNI ya Puma Energy Tanzania
inatarajia kutumia ndege 22 za zamani ambazo zimetengenezwa kati ya miaka ya
1920 na 1930 kutangaza utalii wa Tanzania kwenye nchi mbalimbali duniani.
Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa Kampuni
hiyo, Philippe Corsaletti Dar es Salaam
jana jukumu la kuendeleza utalii ndani ya nchi, linabaki kuwa sehemu muhimu
katika masula ya kijamii.
Alisema katika kufanikisha jukumu hilo
kampuni hiyo itakuwa mwenyeji wa ndege hizo za Vintage Air Rally ambazo zitatua
kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) Novemba 28 zikitoka
Uwanja wa Ndege wa Wilson, Nairobi.
Alisema marubani wa ndege hizo
watakapofika nchini watatembelea mbuga za wanyama kama sehemu ya safari yao,
hivyo Puma inaamini itasaidia kuweka utalii kwenye mtizamo wa
kimataifa zaidi.
Corsaletti alifafanua kuwa ni kwa sababu
ndege hizo zipo kwenye shindano la kuzunguka duniani kuna maelfu ya watu
wanafuatilia.
"Kampuni ya Puma tumejiandaa
kupokea ugeni huu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha huduma zote za kujaza mafuta
ili kuhakikisha urukaji ulio salama. Ndege hizo zinatumia mafuta aina ya Avgas
ambayo kwa sasa ni kampuni ya Puma pekee iliyonayo nchini.
Aliongeza kuwa nchini, ndege hizo
zitajaza mafuta Kilimanjaro, Arusha, Dar es Salaam, Zanzibar, Dodoma na Songwe
kabla ya kwenda Zambia ambako zitapokewa na kuhudumiwa na Puma Zambia.
"Tanzania itaweka historia kwa kuwa
moja ya nchi chache duniani ambako mashindano hayo yatapita. Tunawakaribisha
wananchi katika tukio hili la kihistoria wakati ndege za Vintage zitakapokuwa
zikipita maeneo yenu na kutumia fursa hii kuendeleza utalii," alisema Philippe.
Aliongeza kuwa njia itakayotumika ni
sawa na ufuatishaji wa safari ya Shirika la Ndege la Imperial ya mwaka 1931
"Safari ya Afrika" ambapo ndege itakuwa ikiruka chini kupitia Nile
kutokea Kongo hadi Khartoum, kupitia nyanda za juu za Ethiopia na uwanda wa
chini wa Kenya.
"Baada ya hapo itaondoka tena
kupitia Kilimanjaro hadi Serengeti, na hatimaye kwenye visiwa vya Zanzibar na
hadi chini zaidi, kupitia Zambia, juu ya maporomoko ya Victoria, hadi Bulawayo,
Zimbabwe," alisema.
"Shindano hili lilianza Novemba 12
Crete, Ugiriki na safari yote itachukua siku 35 kupitia nchi 10 za Ugiriki,
Misri, Sudan, Ethiopia, Kenya, Tanzania, Zambia, Zimbabwe, Botswana na Afrika Kusini.
Shindano linalenga kutathmini ujuzi wa marubani husika," alisema.
0 comments:
Post a Comment