Wizara yajipanga kuleta mapinduzi kwenye Kilimo


Enlesy Mbegalo

SERIKALI imesema kuwa itaanza kutoa takwimu za kilimo kwa vifaa vya teknolojia za simu za mkononi na komputa mpakato ili ziweze kupunguza gharama ya kuandaa madodoso.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Meneja wa Takwimu za Kilimo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Titus Mwisomba  wakati wa Mkutano wa siku tano wa  wadau wa  Takwimu za Kilimo Kanda ya Afrika.

Mwisomba alisema kuwa takwimu hizo za teknolojia  zitawasaidia wadau hao wanaoshiriki katika masuala mbalimbali ya  kilimo ili waweze kupata takwimu za kilimo zenye ubora kwa wakati.

“Rasilimali tulizonazo ni ndogo na tumejipanga kuanza kutoa takwimu kwa kutumia teknolojia ili tuweze kupunguza gharama za madodoso na matokeo yaweze kutolewa kwa wakati,” alisema Mwisomba

Aliongeza kuwa takwimu hizo zikitolewa kwa njia ya teknolojia zitasaidia pia kupunguza gharama za tafiti zingine.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk.Frolence Turuka alisema mkutano huo utasaidia  namna ya kuwa na ukusanyaji bora wa takwimu za kilimo.

“Nchi nyingi za Afrika zinategemea sana kilimo labda ni utofauti tu ni kwa kiasi gani, ila Tanzania pato la taifa linategemea kilimo kwa asilimia 30,”alisema Dk. Turuka

Alisema kuna shida ya kuwa na takwimu sahihi  na mkutano huo utasaidia katika kupanga mikakati ya pamoja ambayo itawezesha Nchi za Afrika katika kupanga mikakati ya maendeleo ya kilimo hasa maeneo ya vijijini.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo