Grace Gurisha
WAKILI Alex Mgongolwa ameiomba Serikali imwache huru
aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya kwa madai
kuwa waliomshitaki wameshindwa kukamilisha upelelezi wa kesi inayomkabili ya uhujumu
uchumi.
Katika ombi hilo alilolitoa jana mbele ya Hakimu Mkazi
Mfawidhi, Cyprian Mkeha wakati kesi hiyo ilipotajwa, Wakili huyo alipendekeza
baada ya Kitilya kuachwa, upelelezi uendelee na utakapokamilika, mteja wake
aliyedai kuwa anateseka gerezani kwa miezi minane sasa akamatwe tena.
“Tunaomba Mahakama iweke ukomo katika upelelezi au upande
wa mashitaka ufute kesi hii na watakapomaliza upelelezi wamkamate tena, kwa
sababu tangu mwaka jana wanachunguzwa. Mtu akifikishwa mahakamani lazima hatima
yake ijulikane mapema.
“Mwelekeo wa Jamhuri ni kupoteza mwenendo wa kesi wa
Mahakama, kwa sababu kila siku wanakuja na wimbo wa upelelezi bado, huu wimbo
ni hatari na hauna ukomo,” alidai Mgongolwa.
Alitoa malalamiko hayo baada ya Wakili wa Serikali, Elia
Athanas kuieleza Mahakama kuwa upelelezi bado na timu ya uchunguzi wa kesi hiyo
bado inaendelea nan upelelezi.
Hata hivyo, Hakimu Mkeha alisema jalada linapokosa mtu
maalumu linaweza kupoteza mwelekeo, upande wa Jamhuri unatakiwa kuweka mtu
maalumu atakayeulizwa na kujibu, tofauti na ilivyo sasa kwenye kesi hiyo. Kesi
hiyo iliahirishwa hadi Desemba 2.
Mbali na Kitilya, washitakiwa wengine ni aliyekuwa Mrembo
wa Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare na aliyekuwa mgombea ubunge wa Arumeru
Mashariki, Sioi Solomon wote wakiwa wafanyakazi wa benki ya Standard Chartered.
Mashitaka mengine yanayowakabili katika kesi hiyo mbali
na kutakatisha fedha, ni kutumia nyaraka za kughushi na za uongo, kujipatia
isivyo halali dola milioni 6 za Marekani, sawa na Sh bilioni 12.
Awali, upande wa mashitaka uliiambia Mahakama kuwa katika
tarehe tofauti kati ya Agosti 2012 na Machi 2013 Dar es Salaam, washitakiwa hao
walipanga kwa kushirikiana na watu wengine ambao hawakufikishwa mahakamani,
kutenda kosa la kujipatia fedha kwa udanganyifu kutoka serikalini.
Ilidaiwa kuwa kati ya Agosti 2, 2012 kwenye makao makuu
ya benki ya Stanbic Tanzania Limited, Kinondoni, Sinare akiwa na nia ovu,
alighushi taarifa ya maombi ya fedha ya benki ya Standard Agosti 2, 2012. Kwa
mara ya kwanza washitakiwa hao walipandishwa kizimbani Aprili mosi.
0 comments:
Post a Comment