Moses Ng’wat, Mbeya
UHAKIKI wa vyeti
vya watumishi wa umma unaofanyika nchi nzima, umeacha kilio mkoani Mbeya kwa
watumishi 11 wa Idara ya Afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, ambao
wamefukuzwa kazi baada ya kukutwa na vyeti feki.
Hatua hiyo imechukuliwa wiki chache baada ya Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), kukamilisha uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma mkoani humo.
Hatua hiyo dhidi
ya watumishi hao, imechukuliwa jana katika kikao cha kwaida cha robo ya kwanza
ya mwaka cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo.
Kabla ya kufikia
uamuzi huo, Baraza hilo lilijigeuza kuwa kamati, kwa ajili ya kujadili kwa kina
nidhamu za watumishi wa halmashauri hiyo ambapo wageni wote waalikwa kwenye
kikao hicho walitakiwa kutoka nje.
Baada ya kikao
cha kamati kumalizika na baraza hilo kurejea katika hali yake ya kawaida,
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Francis Mtega, alitangazia umma
azimio la halmashauri la kuwafukuza kazi watumishi hao.
“Baraza la
Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali limeridhia kufukuzwa kazi kwa
watumishi hao baada ya Baraza la Mitihani Tanzania kutuhakikishia kuwa vyeti
vyao ni feki,” alisema Mtega.
Aliwaasa vijana
wilayani Mbarali kusoma kwa bidii ili wapate vyeti halali vya kitaaluma ambavyo
havitawasababishia matatizo katika siku za usoni wakiwa kwenye ajira zao.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Kivuma Msangi, alisema watumishi
hao walibainika kuwa na vyeti feki baada ya utekelezaji wa agizo la Rais John
Magufuli kutaka ufanyike uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma.
Alisema hatua
iliyochukuliwa ya kuwafukuza kazi watumishi hao ni ya kinidhamu, lakini bado
watumishi hao watachukuliwa hatua za kisheria kwa kuwa tuhuma zao pia zinaangukia
kwenye makosa ya jinai.
Mkurugenzi huo
hakutaka kuwataja watumishi hao kwa madai kuwa bado mchakato wa kuwachukulia
hatua za kisheria unaendelea, ili wawajibishwe kwa makosa ya kijinai kama
yatathibitika.
0 comments:
Post a Comment