Mwigulu Nchemba |
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu
Nchemba amesema watumishi waliopo ndani ya wizara yake ambao si askari wana
matatizo na wanawakwamisha askari.
Mwigulu aliyasema hayo juzi jijini Dar
es Salaam wakati akizungumza na wafanyakazi wa Idara ya Uhamiaji. Alisema aliulizwa
swali bungeni kuhusu askari wapya waliokaa bila kupata mshahara kwa wakati na
alivyofuatilia alibaini tatizo lipo kwa watumishi upande wa utawala.
Alisema askari hao wapya ambao wengi
wamepangiwa maeneo ya nje ya mji wamepata shida kutokana na uzembe wa watumishi
hao.
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Afisa
Utawala Mkuu wa Uhamiaji, Mulegi Majogoro alisema askari hao wapya ambao
walikuwa 297 waliochelewa kupata mshahara wao baadhi yao majina yalikosewa.
Alisema kulikuwa na tatizo la mtandao na kukatika kwa umeme ndiyo maana
wakachelewesha taarifa zao.
Baada ya maelezo hayo Mwigulu alisema “Nyie
watu wa utumishi mna matatizo nashangaa kwanini mnabisha, mnawasumbua askari
katika malipo kwani inajulikana kuwa kila askari ambaye anaishi nje ya kambi
anapewa asilimia 15 ya fedha yake ya mshahara ili akalipe pango lakini mmekuwa
mkiwababaisha.’’
‘’Hivi mnatoa wapi ujasiri wa kuwaibia
askari wetu ambao mnajua wanafanya kazi kwa shida? Unakuta mtu alikuwa analipwa
mshahara wa Sh 300,000 mkawa mnampa asilimia 15 ya mshahara wake kama pango na
akapandishwa cheo mshahara ukazidi hadi 1,000,000 lakini hamjamfanyia
marekebisho katika fedha anayotakiwa kupewa mnampa ile ile,’’aliongeza
Alisema watumishi hao wanaona kwamba
askari ni watu wa kawaida lazima waishi kimsoto msoto wakati wanafanya kazi
kubwa katika mazingira magumu.
“Watu hawa wanafanya vibaya sana kwani
ikitokea maofisa wenzao ambao sio askari wamepandishwa cheo wanafanya taratibu
zao za malipo mapema na kiwango cha
mshahara kubadilika lakini ikitokea askari kapandishwa cheo atakaa kipindi
kirefu anasota kusubiri wabadilishe’’
Aliwaomba watumishi wote wa idara hiyo
wamuone ofisini kwake leo saa 2:00 asubuhi.
Wakati huo huo Mwigulu aliitaka Idara ya
Uhamiaji kufanya kazi kwa uadilifu na kutolinda watu wasiokuwa na vibali vya
kuishi nchini.
“Tutekeleze sheria katika kupambana na
watu wanaoishi nchini kinyume na sheria, wasiokuwa na sifa lakini pia tusifanye
kazi ya kusaidia wanaotaka kutapeli ambao wanaanza kufanya biashara na wageni
inapofikia katika hatua nzuri wanataka kuwatapeli wanakimbilia kwenu kuwaambia
muwafukuze sio raia hii si sawa’’alisema Mwigulu
Pia aliahidi kutatua changamoto ya
wateja wanaotafuta hati za kusafiria kuchelewa katika dirisha la malipo wakati
walishalipa fedha benki kwa kuanza utaratibu wa kutumia mashine za
kielektronik,kuangalia upya tafsiri ya sheria ambayo inawatoa baadhi ya
watanzania ambao walizaliwa nchini na hawana uraia wan chi yoyote.
0 comments:
Post a Comment