Magufuli ampa jeuri Makonda

Salha Mohamed

Rais John Magufuli
Wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akizongwa na vyombo vya habari kwa kauli zilizodaiwa si za kiongozi wa hadhi yake, Rais John Magufuli, amemuhakikishia kiongozi huyo kuwa anamuunga mkono kwa asilimia 100.

Akizungumza kwa simu iliyounganishwa na vipaza sauti na kusikika moja kwa moja kwa wananchi katika mkutano wa hadhara, uliorushwa moja kwa moja na Televisheni ya Clouds jana Ubungo Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema anatamani wakuu wa mikoa wote wangekuwa kama Makonda.

“Natamani wakuu wa mikoa wote wangekuwa kama wewe katika kusikiliza na kutatua kero na changamoto za wananchi, na kupongeza sana.

“Wananchi wana kero nyingi sana, lakini viongozi wao wangekuwa wanawasikiliza hata maswali wanayouliza hapo yasingeulizwa, nakupongeza sana Mkuu wa Mkoa natamani na viongozi wengine wangeiga,” alisema Rais Magufuli.

Makonda aliyeanza ziara yake Novemba 19 mwaka huu akiwa anasikiliza na kutatua changamoto za wananchi katika wilaya tano jijini humo, alihakikishiwa jana kuwa ziara hiyo ina baraka zote za Rais.

Ziara hiyo iliibua migogoro na changamoto nyingi za wananchi ambazo alizitatua na zingine alichukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuagiza kukamatwa kwa baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa na kuchunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Magufuli katika simu hiyo alisema juhudi anazozifanya Makonda ni za kuigwa na viongozi wengine katika mikoa yao kwani zinasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Hifadhi ya barabara
Kuhusu hifadhi ya barabara ambayo iliibua mjadala kati ya wananchi waliojenga katika hifadhi waliokuwa wakigoma kuvunjia nyumba zao na Wakala wa Barabara (Tanroads), Rais Magufuli alisisitiza kuwa Serikali itavunja majengo yote yaliyokuwa kwenye hifadhi hata likiwa jengo la Shirika la Umeme (Tanesco).

Alisema suala la barabara kutoka Ubungo hadi Ruvu, alishawahi kutolea ufafanuzi mara kadhaa kwani akiwa Waziri wa Ujenzi mwaka 1997, kulitokea migogoro kama hiyo.

“Nawaeleza wananchi kuvunja kupo pale pale kwasababu sasa hivi tumepata Sh bilioni 67 za kujenga barabara ya juu pale Ubungo, itakuwa ya gorofa mbili au tatu na ili kurahisisha usafi pale, kuna majengo ya ghorofa yatavunjwa bila fidia hata kama litakuwa jengo la Tanesco,”alisema.

Alisema lazima wazingatie sheria, lakini kwasababu wameshalifafanua vema wananchi wakiona wanaonewa waende mahakamani.

“Wakati tunataka kupanua barabara hiyo kutoja Ubungo kwenda Kibaha, palitokea malalamiko ya aina hiyohiyo na tukapelekwa mahakamani.

“Ilikua kesi namba 137, kesi hiyo tulishinda ilikuwepo Mahakama Kuu baada ya kutoa uamuzi wa pamoja kuhusu maeneo yaliyopo katiia hifadhi ya barabara,”alisema.

Alisema kutokujua sheria hakumfanyi mwananchi kuvunja sharia, ndio maana baada ya ushindi ule kutoka Mahakama Kuu, walichukua hatua ya kubomoa nyumba zote zilizokuwa katika hifadhi ya barabara.

Rais Magufuli alifafanua kuwa bomoabomoa hiyo ilifanyika kwa mujibu wa sheria hiyo ambayo ilitungwa mwaka 1932, ikafanyiwa marekebisho mwaka 1949 ikafanyiwa tena marekebisho 1954 na mwaka 1965.

“Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Vijiji namba tano ya mwaka 1999 na Sheria ya Mipango Miji na Matumizi ya Ardhi ya mwaka 2007, zote zinatambua hifadhi ya barabara.

“Kwa barabara ya Dar es Salaam kwenda Kibaha iliachwa kwa upana ule ndio maana upana wa Ubungo mpaka Sanamu la Askari Samora jijini ni meta 22.5 kila upande.

“Baada ya Ubungo katika jengo la Tanesco, upana unaongezeka ukienda pale Kilometa 10, upana unaongezeka zaidi ukifika kwenye daraja la Kibaha unarudi kwenda kwenye meta 20.5 hadi kwenye daraja la treni upana tena unaongezeka baada ya daraja hilo upana ni meta 20.5 hadi Mwanza,”alisema.

Alisema barabara zote kuu upana ni meta 20.5 na kutoa mwito kwa wananchi wazingatie sheria na kusisitiza kuwa sheria ni msumeno.

Rais Magufuli alisema ni wajibu wa Serikali kusimami sheria, lakini endapo wananachi wanaona sheria haifai, ni kiasi cha kwenda kulishauri Bunge libadilishe sharia, ili barabara ya Ubungo iwe sentimeta tano zitakazopitisha bajaji pekee.

“Ukweli unabaki palepale kwamba sheria ipo na haijawahi kubadilishwa. Mimi naipongeza (Tanroads) kwa kusimamia sheria kwasababu itafika wakati tutajikuta Tanzania hatuna barabara,”alisema.

Alisema ndio maana hadi sasa ofisi ya Tanroads iliyokuwepo Ubungo alienda mwenyewe kuivunja kwa kuwa ilikuwa hifadhi ya barabara.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo