Mwandishi Wetu
MWILI wa mtoto Justine Chedega (6) aliyefariki dunia
akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Kitengo Cha Mifupa
(MOI) umetelekezwa mochari na familia yake kwa takribani siku 24.
Taarifa ambazo JAMBO LEO, ilizipata jana kutoka Moi,
zilisema mtoto huyo alifariki dunia Oktoba 28 wakati akitibiwa baada ya kupata
ajali ya kugongwa na pikipiki.
“Mtoto huyo alifikishwa hapa Oktoba 23 na kufariki dunia
Oktoba 28, hadi leo mwili wake uko mochari, ndugu zake hawaonekani,” kilisema
chanzo hicho.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Justine alifikishwa
hospitalini hapo akitokea hospitali ya Temeke alikofikishwa awali baada ya ajali.
Chanzo cha kutelekezwa kwa mwili wa mtoto huyo kinatajwa
kuwa utata wa jina aliloandikishwa baada ya kufikishwa hospitalini.
Kwa mujibu wa taarifa za kiuchunguzi ndani ya hospitalini
hiyo, Justine alifikishwa MNH na mtu anayejitambulisha kuwa Abdallah Said mkazi
wa Kitunda Mwanzo, Temeke.
Uchunguzi unaonesha kuwa Said ni baba wa kambo wa Justine
ambaye baada ya kumfikisha na kufungua jalada la matibabu, alimsajili kwa jina
la Justine Abdallah Said.
Taarifa zilipasha kuwa baada ya kupata taarifa za kifo cha
mtoto wake, baba mzazi, Robert Chedega wa Dodoma alijitokeza kutaka kuchukua
mwili, lakini alipobaini jina la pili limebalishwa, alisita kufanya hivyo na
kuondoka.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Chedega alisema jina sahihi
la mtoto wake ni Justine Robert Chedega na kupinga jina alilolikuta akitaka
kuchukua mwili alitakiwa kuandika barua maalumu kuomba kibali apewe.
Habari zilipasha kuwa baada ya kuelezwa hivyo na maofisa
wa Moi, Chadega alikataa na kuondoka bila kuacha mawasiliano na hadi jana
hakuna aliyejitokeza kuchukua mwili wa mtoto huyo.
Baba wa kambo alipotafutwa kupitia namba ya simu
aliyoacha MNH kwa kuwa ndiye aliyemfikisha mtoto huyo hospitalini, simu yake
haikupatikana.
Ofisa Habari wa Kitengo cha Moi, Jumaa Almasi
alipotafutwa ili kupata ufafanuzi wa tukio hilo, simu yake iliita mara kadhaa
bila majibu.
Hata hivyo, JAMBO LEO inaendelea kufuatilia tukio hilo
kutoka kwa wahusika.
0 comments:
Post a Comment