Dotto Mwaibale
George Simbachawene |
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, amesema ili kusimamia mabadiliko na
kuleta maendeleo ya nchi na maadili, kunahitajika kiongozi mbabe na mtemi.
Simbachawene alisema hayo jana wakati akifunga mafunzo ya
uongozi na maadili kwa wahitimu 47 wazalendo kwenye Chuo cha Kumbukumbu ya
Mwalimu Nyerere, baada ya kumaliza ujenzi wa kujitolea kwa mwezi mmoja Mkuranga
mkoani Pwani.
Alisema ili kusimamia mabadiliko na maendeleo, nchi
inatakiwa kuwa na mtu mbabe na mtemi na si kutegemea kundi fulani la watu,
kwani kufanya hivyo, kila kundi litahitaji kupendelewa baada ya kujiona bora
kuliko lingine.
Alisema bila kuwa na viongozi wenye maadili, nchi haiwezi
kusonga mbele kwani tangu kuachwa mfumo wa vijana kujiunga na Jeshi la Kujenga
Taifa (JKT), ambako kulitolewa mafunzo ya maadili, athari zake zilijitokeza.
Akifafanua athari hizo, Simbachawene alisema ndipo kwa
kipindi cha miaka 20 CCM ilivamiwa na matajiri wakitaka nafasi za uongozi wa
ngazi za ubunge, urais na ujumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama.
"Napenda kusema kuwa tunahitaji mabadiliko makubwa
ya kufumua chama chetu hasa katika mfumo mzima wa kupata viongozi, kwani uliopo
umetufanya tupoteze baadhi ya nafasi katika majimbo na hata kwenye uchaguzi
mdogo.
“Kutokana na mfumo mbaya tulishindwa baada ya wanachama
wetu kumpigia kura mtu mwingine kwa hasira, huku vikao vyote vikiendeshwa kwa
misingi ya fedha," alisema Simbachawene.
Alisema ilifika hatua kila jambo lilikuwa haliwezi
kufanyika bila kuomba ufadhili kwa matajiri ambao wengi wao ndio walikuwa
wakwepa kodi.
Aliongeza kuwa watumishi wa umma wamekuwa wakilalamika
kuwa hali ya maisha ni ngumu huku wengine wakisema Hazina hakuna fedha, wakati
hakuna hata mwezi ambao mtumishi amekosa mshahara.
Alisema pengine hali hiyo inatokea kwa kuwa watumishi hao
walikuwa wakitegemea kitu kingine mbali ya mshahara, baada ya mianya hiyo
kufungwa, wanalalamika.
Aliongeza kuwa awali bandarini kulikuwa na pilikapilika
nyingi za mlundikano wa kontena na magari, lakini makusanyo yalikuwa hayafiki
hata Sh bilioni moja kwa mwezi, lakini sasa pilikapilika hazipo zinakusanywa Sh
trilioni moja “hii inaonesha kodi ilikuwa hailipwi ipasavyo”.
Alisema nchi ilifikia pabaya, kwani kila sehemu kulikuwa
na madalali iwe hospitali, ofisi za Serikali, mahakamani na hata kwenye kupata
vyeo lakini hivi sasa mianya hiyo
imezibwa.
Alisema anachokifanya Rais John Magufuli ni mabadiliko
ili watu waache kuishi kwa mazoea na nchi ipige hatua katika masuala yote.
Simbachawene alisema changamoto kubwa iliyopo ni
kuchanganya sera za siasa na za uongozi, jambo linalosababisha mambo mengine
kushindwa kusonga mbele.
Mkuu wa Chuo, Profesa Shadrack Mwakalila alisema baada ya
kuona mmomonyoko wa maadili miongoni mwa Watanzania hasa kwa baadhi ya viongozi,
chuo kimeona ni vema kurejesha mafunzo ya uongozi na maadili ili kupunguza kama
si kumaliza kasi ya mmomonyoko wa maadili.
0 comments:
Post a Comment