Moses Ngwat, Mbarali
MWENYEKITI wa
Kijiji cha Nyeregete, wilayani Mbarali, Moses Fute, anatuhumiwa kuuza ardhi
inayomilikiwa na kijiji hicho kwa watu binafsi, wakiwemo viongozi wa Serikali,
askari polisi na mahakimu, huku mwenyewe akijimilikisha ekari 300.
Ardhi hiyo yenye
ukubwa wa ekari 2671.4 ilitengwa na kijiji hicho kwa ajili ya mradi wa
kuwaendeleza vijana katika kilimo cha mpunga kwa kuwagawia ekari tano kwa kila
kijana ambaye alihitaji kujihusisha na shughuli za kilimo.
Hata hivyo, Mkuu
wa Wilaya ya Mbarali, Ruben Mfune ameagiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya mwenyekiti
huyo na wote waliohusika na uporaji huo wa ardhi kwa kuwa ndio wamekuwa chanzo
cha migogoro katika wilaya hiyo.
Akiwahutubia wananchi
wa kijiji hicho katika mkutano wa hadhara juzi, mkuu huyo wa Wilaya ya Mbarali
alitoa siku 14 kwa wataalamu wa ardhi wilayani humo na viongozi wa Mamlaka ya
Mji mdogo wa Rujewa kupima upya eneo hilo na kuligawa kwa wananchi.
“Nimeagiza hatua
zichukuliwe kwa wale wote waliohusika na hujuma hizi, lakini pia nimeagiza hadi
kufikia tarehe 10 mwezi ujao (Disemba) viongozi wa mamlaka na wataalamu wa
ardhi wawe wamemaliza kupitia upya mchakato wa ugawaji ili kila mwananchi apate
ardhi ya kilimo” alisema Mfune.
Kadhalika, mkuu
huyo wa wilaya amewataka wale wote waliouziwa mashamba na kuanza shughuli za
kilimo katika eneo hilo kusitisha mara moja na kwamba atakayekutwa akijihusisha
na shughuli yeyote katika eneo hilo atakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Awali, akielezea
sakata hilo Kaimu Ofisa Mtendaji wa Mamlaka ya Mji wa Rujewa, Fortnatus
Mjengwa, alisema sakata hilo la kuuzwa kwa aridhi ya kijiji
lilitokea kabla ya kijiji hicho kuvunjwa na kujumuishwa kwenye eneo la Mamlaka
ya Mji mdogo wa Rudewa.
Hata hivyo,
Mjengwa alisema kuwa ardhi hiyo iliyouzwa ilihusisha vitongoji vinne na kwamba
tayari wamemaliza kuhakiki na kuyapima maeneo yote yaliyouzwa katika vitongoji
hivyo na pindi mchakato wa kuorodhesha majina ya wanakijiji wote
wenye uhitaji wa mashamba ukikamilika watayagawa.
Akifafanua zaidi
alisema baada ya kupima upya ilibainika kuwa kitongoji cha Maborishi kina ekari
1121 zilizouzwa, kitongoji cha Mangenyu ekari 390 ambazo zilitengwa kwa ajili
ya wafugaji, Katenge ekari 337 na Kitongoji cha Nyamto ekari 823 ambazo nyaraka
za waliouziwa zinaonyesha vigogo mbalimbali wa serikali.
“Kuna watu
wameuziana ekari 500 wakati sheria ya ardhi iko wazi juu ya nani ana mamlaka ya
kuuza eneo kubwa kama hilo. Kibaya zaidi walionunua wapo waheshimiwa mahakimu,
watendaji wa halmashauri, hadi viongozi wa polisi na ndio maana kila wananchi
walipojaribu kulalamika mwisho wake ilikuwa ni kukamatwa na kuwekwa ndani”
alifafanua Mjengwa.
Hali hiyo ya
kurudishwa mikononi mwa kijiji na kuamuliwa kugaiwa kwa wananchi ilipokerewa
kwa furaha kubwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo na kumuomba Mkuu wa
Wilaya hiyo kuendelea na hatua hiyo katika maeneo mengine yenye migogoro.
0 comments:
Post a Comment