Leonce Zimbandu
Anthony Lusekelo
|
MCHUNGAJI wa Kanisa la Maombezi (GRC)
Ubungo Kibangu, Anthony Lusekelo, maarufu Mzee wa Upako amesema mawaziri wakuu
wa zamani Edward Lowassa, na Fredrick Sumaye pamoja na kada mkongwe wa CCM,
Kingunge Ngombale Mwiru hawakukikimbia chama
hicho tawala, bali wamemkimbia ‘mtu’
Akitoa mahubiri jana katika kanisa lake
lililopo Ubungo Kibangu Dar es Salaam, siku chache baada ya kuhojiwa na Polisi
kwa tuhuma za kutoa lugha ya matusi kwa jirani zake eneo la Kawe, Lusekelo
amesema, siyo rahisi kwa vigogo hao watatu kukikimbia chama kilichowalea bali
wamemkimbia mtu.
“Si rahisi kukimbia chama kilichowafinyanga na kuwalea katika safari yao yote ya siasa, hawa
wamesoma alama za nyakati, wakaamua kukaa pembeni,” alisema huku mamia ya
waumini wake wakimshangilia.
Lusekelo ambaye hakutaja mtu
waliyemkimbia wanasiasa hao wakongwe, alisema kwa kuwa viongozi wa dini
wamefanikiwa kuunganisha taifa kwa kuhubiri upendo na amani, Watanzania wasikubali
kugawanywa kwa misingi ya siasa.
“Unajua siku moja niliuzwa mimi ni chama
gani maana sieleweki, nadhani ningekuwa CCM nisingekamatwa na polisi,” alisema.
Lusekelo ametoa kauli hiyo ikiwa umepita
zaidi ya mwaka mmoja tangu Lowassa, Sumaye na Kingunge walipohama CCM, huku
kila mmoja akitoa sababu zake kujiengua kutoka chama hicho tawala.
Julai 29, alipokuwa akitangaza kujiunga
na Chadema baada ya kujitoa CCM, Lowassa alitaja sababu mbalimbali ikiwamo mchakato
wa kuteua wagombea urais kugubikwa na mizengwe, ukiukwaji wa maadili, uvunjaji
wa Katiba na taratibu za uchaguzi za chama hicho.
“Niliwekewa mizengwe na kuzushiwa
majungu na uongo mwingi, zaidi ya hayo uchaguzi ulisimamiwa kwa upendeleo
dhahiri na chuki iliyokithiri dhidi yangu. Kikatiba, Kamati ya Maadili si
chombo rasmi na haina madaraka ya kuchuja na kupendekeza majina miongoni mwa
wale wanaoomba kugombea Urais kupitia CCM,” alisema na kuongeza:
“Kilichotokea Dodoma ni kupora madaraka
ya Kamati Kuu na kukiuka Katiba ya CCM, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu
viliitishwa na kuburuzwa ili vitekeleze azma ya watu binafsi pasipo kujali
demokrasia, katiba, kanuni na taratibu za uchaguzi ndani ya CCM.
Alisema: “CCM siyo mama yangu wala baba
yangu ni wakati wa kutekeleza majumu kwa wanachi.”
Agosti22, mwaka jana naye Sumaye
alipokuwa akitangaza kuhama CCM mbele ya viongozi wa Ukawa na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam, alisema:
“Nimeamua kujiunga na Ukawa ili kusaidia
nchi iende kwa kasi kubwa katika kuleta maendeleo ya wananchi ambao wamechoka
na wanataka mabadiliko ambayo ni ya dhahiri.”
Kwa upande wake, Kingunge aliyehama CCM Oktoba 5, mwaka jana alisema chama hicho kimepoteza dira na mwelekeo.
“Nimeamua kuchukua uamuazi mgumu kwa
kusoma alama za nyakati kutokana na anguko la CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao,”
alisema.
0 comments:
Post a Comment