TRA yapoteza Sh bilioni 400


Mwandishi Wetu

WAKATI Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ikimaliza siku ya pili bila Bodi ya Wakurugenzi, taarifa mpya zinaonesha Mamlaka hiyo imeshindwa kukusanya Sh bilioni 401, katika miezi mitatu ya kwanza ya Bajeti ya Serikali.

Juzi asubuhi, Rais John Magufuli ambaye Serikali anayoongoza imefanikiwa katika ubanaji matumizi, alivunja Bodi ya Wakurugenzi ya TRA na kumfuta kazi Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bernard Mchomvu katika taarifa ambayo haikueleza  sababu.

Baadhi ya vyombo vya habari katika kubashiri sababu za uamuzi huo, vilifanya tathimini ya makusanyo ya mapato ya Septemba yaliyoonesha kuwa Serikali ilitarajia kukusanya Sh trilioni 1.37, ambayo ni pungufu ya matarajio ya makusanyo kwa asilimia 84.3.

Upotevu bil. 400/-

Hata hivyo, taarifa sahihi inaonesha kuwa Septemba, Serikali ilitarajia kukusanya Sh trilioni 1.67, lakini iliambulia Sh trilioni 1.4 tu.

Hesabu za makusanyo ya miezi mitatu ya kwanza ya Bajeti ya Serikali, katika taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya mapitio ya uchumi ya kila mwezi iliyotoka mwezi jana, imeonesha hali si nzuri.

Kwa mujibu wa hesabu hizo, katika miezi hiyo ya Julai, Agosti na Septemba, Serikali ilitarajia kukusanya Sh trilioni 4.34, lakini TRA ilikusanya Sh trilioni 3.94 tu.

Mchanganuo wa makusanyo umeonesha kuwa katika Bajeti ya Serikali ya 2016/17 makusanyo ya kodi yalipaswa kuwa Sh trilioni 15.07 na kati ya hizo, katika miezi mitatu ya mwanzo, TRA ilipaswa kukusanya Sh trilioni 3.5, lakini ikakusanya Sh trilioni 3.45 tu.

Katika mapato yatokanayo na ushuru wa bidhaa kutoka nje ya nchi, Bajeti ya Serikali 2016/17 iliweka matarajio ya makusanyo ya Sh trilioni 5.67 na katika miezi hiyo mitatu, matarajio yalikuwa makusanyo ya Sh trilioni 1.38, lakini TRA ikakusanya Sh trilioni 1.33 tu.

Kuvuka matarajio

BoT katika taarifa yake, ilieleza kuwa ushuru unaotozwa katika mauzo ya bidhaa na huduma za ndani na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa mwaka huo wa bajeti ya Serikali matarajio ni kukusanya Sh trilioni 2.92 na katika miezi hiyo mitatu, matarajio ilikuwa kukusanya Sh bilioni 658.6 na hapo ndipo TRA ilipovuka matarajio kwa kukusanya Sh bilioni 723.09.

Kodi ya mapato kwa mwaka 2016/17 Serikali ililenga kukusanya Sh trilioni 5.31 na katika miezi hiyo mitatu ya mwanzo, matarajio ilikuwa makusanyo ya Sh trilioni 1.2 lakini TRA ikakusanya Sh trilioni 1.15 tu.

Katika kodi zingine, Serikali ililenga kukusanya Sh trilioni 1.15 kwa mwaka wa fedha 2016/17 na katika miezi mitatu ya kwanza, ilitarajiwa kukusanya Sh bilioni 254.9 lakini TRA ikakusanya Sh bilioni 247.7 tu.

Upotevu mkubwa

Mapato yasiyo ya kodi, Serikali kwa mwaka ilitarajia kukusanya Sh trilioni 2.71 na katika miezi mitatu ya mwanzo ilitarajia kukusanya Sh bilioni 678.13 lakini TRA ikakusanya Sh bilioni 357.35 tu, hali inayoonesha ndiko kwenye upotevu mkubwa wa mapato.

Katika mapato kutoka vyanzo vya serikali za mitaa, kwa mwaka wote wa fedha Serikali ilitarajia kukusanya Sh bilioni 665.41 na katika miezi mitatu, ilitarajia makusanyo ya Sh bilioni 166.35 lakini TRA ikakusanya Sh bilioni 133.96 tu.

Matumizi yafekwa    

Hali hiyo ya makusanyo hafifu ya TRA, ilisababisha Serikali kupunguza matumizi ili kuendana na hali ya mapato, ambapo katika miezi hiyo mitatu ilitarajia kutumia Sh trilioni 6.34 lakini ikajifunga mkanda na kutumia Sh trilioni 3.85.

Moja ya maeneo yaliyopata shida katika matumizi ni miradi ya maendeleo, ambako katika miezi hiyo ilitakiwa kutumia Sh trilioni 1.4 lakini Serikali ikajikuta ikipeleka Sh bilioni 862.7.

Panga lingine lililopigwa ni katika matumizi ya kawaida, ambapo Serikali ilipanga katika miezi hiyo mitatu kutumia Sh trilioni 1.04, lakini ikatumia Sh bilioni 724 tu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo