Jaji Mkuu |
HATIMAYE Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na
Uhujumu Uchumi maarufu Mahakama ya Mafisadi, imetoa masharti ya dhamana kwa
wafanyabiashara wanaokabiliwa na kesi ya kukutwa na nyavu haramu za kuvulia
samaki zenye thamani ya Sh bilioni 7.4.
Katika dhamana hiyo, Wafanyabiashara hao Ally Raza (34),
ambaye ni raia wa India na Jeremah Kepenge (40) ambaye ni Mtanzania, wametakiwa
kuweka fedha taslimu Sh bilioni 6.9 au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Awali washitakiwa hao walipeleka maombi ya dhamana katika
mahakama hiyo, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kueleza kuwa haina
mamlaka ya kutoa dhamana hiyo.
Akitoa masharti ya dhamana hiyo jana Jaji Rehema Mkuye
alisema Kepenge anatakiwa kuweka fedha taslimu Sh bilioni 4.4 au hati ya mali
isiyohamishika yenye thamani hiyo na Raza atatakiwa kuweka Sh bilioni 2.5 au
hati.
Katika masharti mengine, washitakiwa hao wanatakiwa kuwa
na wadhamini wawili kwa kila mmoja ambao ni watumishi umma na pia wasitoke nje
ya Dar es Salaam bila kibali kutoka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya
Kisutu.
Aidha wametakiwa kukabidhi hati zao za kusafiria nakuripoti
mara moja kwa wiki katika Kituo cha Polisi cha Bandari.
Jaji Mkuye alifafanua kuwa ili washitakiwa wawe nje kwa dhamana
hiyo, wadhamini na hati vinatakiwa kuhakikiwa katika Mahakama ya Kisutu, kesi
ya msingi inaposikilizwa.
Awali, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), alipinga washitakiwa
hao kupewa dhamana akidai yamefunguliwa kwenye Mahakama isiyo sahihi.
Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo, mvutano mkali
wa kisheria uliibuka baina ya upande wa mashitaka na utetezi kuhusu tafsiri ya
Mahakama Kuu.
0 comments:
Post a Comment