Immaculate Ruzika
SIKU moja baada ya kuripotiwa kuwa kiwanda cha saruji cha
Dangote kimefungwa, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), limesema linafanya
jitihada za kuhakikisha kiwanda hicho kinatumia umeme wa gesi kwa uzalishaji.
Taarifa za kufungwa kwa kiwanda hicho zilitolewa jana kwenye
vyombo vya habari, zikieleza kuwa kimefungwa kutokana na gharama kubwa ya
utumiaji jenereta kuzalisha saruji.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa TPDC,
Kapuulya Musomba alisema walizungumza na Dangote
na kukubaliana kutumia umeme wa gesi unaozalishwa Mtwara.
“Mimi nashangaa kuna taarifa zinazushwa, kuwa sisi TPDC
ndio tumesababisha Dangote kufunga kiwanda, nasema si kweli sasa hivi tuko kwenye
jitihada za kuhakikisha kiwanda kinatumia umeme wa gesi ya Mtwara,’’ alisema.
Musomba alisema Dangote imekuwa ikifanya mazungumzo na
TPDC kwa muda mrefu kuhusu bei ya gesi asilia, ambapo iliomba ipewe bei ndogo,
ambayo ndiyo inayolipiwa kununulia gesi ghafi kutoka kisimani.
Aidha, Musomba alisema TPDC haiwezi kuuza gesi asilia kwa
bei ya kisimani, kwani kuna gharama zinazoongezeka katika kuisafisha na
kuisafirisha.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alitabanaisha kuwa TPDC
imefanya majadiliano ya mkataba wa awali na kiwanda hicho kwa ajili ya kukiuzia
gesi asilia itakayotumika kuzalisha umeme utakaotumiwa na kiwanda.
Musomba aliongeza kuwa inatarajiwa hadi Januari miundombinu
ya gesi itakuwa imeunganishwa na mitambo ya kufua umeme, utakaotumiwa na
kiwanda.
Kiwanda hicho kinamilikiwa na mfanyabiashara maarufu wa
Nigeria, Aliko Dangote.
0 comments:
Post a Comment