Mwijage: Nitakufa na mtu


Immaculate Ruzika

Charles Mwijage
WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, amewaambia makamishina wa ardhi kuwa hatakubali kuondoka peke yake kama italazimika atumbuliwe.

Mwijage alisema hayo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizindua Kitengo cha Huduma ya Pamoja Mahala  pa Kazi cha Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

‘Sitakubali kuondoka peke yangu, ikitokea nimetumbuliwa basi mjue nitaanza na nyie, kabla mimi sijatumbuliwa’’, alisema.

Kauli ya Mwijage imefuatia malalamiko yanayokuwa yakitolewa na wawekezaji kuwa wakiomba ardhi kwa jili ya kuwekeza wanasumbuliwa.

Waziri huyo alisema kuwa maafisa hao wanatakiwa kuwajibika na siyo kujiona miungu watu ili kuweza kufikia lengo la Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Mwijage aliweka bayana kuwa usumbufu huo sio tu kwenye ardhi, hata kwenye kupata leseni ya biashara ni shida, kibali cha kuishi nchini mambo yale yale, hivyo wawekezaji wakiona usumbufu wanakimbia.

Aidha Mwijage aliwaomba watendaji wa Serikali wanaoshughurika na wawaekezaji, wafanye majukumu yao, kwani hivi sasa Tanzania kuna viwanda 1845, ambavyo vinatakiwa viongezeke ili kupanua wigio wa ajira kwa vijana.

‘’Naona watu mnashangaa ninasema Tanzania tuna jumla ya viwanda 1845, ambavyo ni viwanda vidogo, vya kati na vile vikubwa’’, alisema.

Waziri huyo alisema kuwa wameamua kuanzisha huduma hiyo TIC ili iwe rahisi kuwahudumia wawaekezaji, kwani kila anachohitaji kuhusu uwekezaji atakipata hapo.

Alisema katika huduma hiyo kutakuwa na watu wa Uhamiaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), BRELA, Shirika la Viwango Tanzania (TBS),  na  Ardhi, ili muwekezaji atakapofika TIC awe na uhakika wa kumaliza mahitaji yake yote yanayotakiwa.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa TIC, Cliford  Katondo alisema kuwa lengo la kuanzisha huduma hiyo kwa wawekezaji ni kutaka kupanua wigo katika sekta hiyo.

“Sisi tunatimiza agizo la rais John Magufuli ambaye alisema Tanzania ya sasa ni ya viwanda, hivyo tumeona tutengeneze mazingira  mazuri ya kuwakaribisha wawekezaji,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema huduma za mahala pamoja zilianzishwa chini ya Sheria ya Uwekezaji Namba 26 ya mwaka 1997 ambayo iliweka utaratibu wa utoaji vibali na leseni pamoja ili kumrahisishia mwekezaji kupata huduma hiyo kwa urahisi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo