Hussein Ndubikile
Profesa William Anangisye |
WAHITIMU wa Shahada ya Ualimu nchini
wameaswa kuacha kutoa adhabu kali ya viboko kwa wanafunzi na badala yake
wajikite katika maadili na miiko ya
taalima hiyo ili kuzalisha kizazi chenye tija kimaendeleo.
Wosia huo ulitolewa juzi Dar es Salaam
na Rais wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (DUCE), Profesa
William Anangisye kwenye mahafali ya tisa ya chuo hicho.
Alisema walimu watakaoajiriwa,
wanatakiwa kufuata maadili, kwani kuna kasumba imejengeka kuwa adhabu kali za
viboko dhidi ya wanafunzi ndiyo njia pekee ya kuwarekebisha, huku akisisitiza kuwa
kufanya hivyo si suluhisho la mwanafunzi kuzingatia masomo.
"Pale inapobidi kutoa adhabu kwa
wanafunzi zingatieni taratibu, kanuni na sheria, mnapaswa kuelewa kuwa viboko
si njia pekee ya kumrekebisha mwanafunzi, ninyi hapa hamjapigwa kiboko hata
kimoja tangu muanze masomo yenu, leo mnahitimu mkiwa wabobezi katika fani
zenu," alisema.
Profesa Anangisye aliwataka wahitimu hao
kufikiria kujiajiri katika shughuli zinazoendana na tasnia walizosomea na
ujasiriamali badala kusubiri Serikali iwaajiri.
Aliwataka waache kukaa bila kazi, kwani
ndio chanzo cha kujiingiza kwenye matendo yasiyofaa ambayo mwisho wake ni mbaya
yakiwamo ya matumizi ya dawa za kulevya, wizi na ujambazi na kutoshiriki
uvunjifu wa amani kwa kutumiwa na wanasiasa.
Katika mahafali hayo jumla ya wahitimu
1,179 walitunukiwa shahada za awali katika fani mbalimbali na 80 Shahada za
Uzamili katika Elimu hivyo jumla yao kuwa 1,259, kati yao wanaume ni 429 na
wanawake ni 840.
Alifafanua kuwa chuo hicho kinakabiliwa na
changamoto za uhaba wa mabweni ya wanafunzi ambapo kina nafasi 412 za bweni
huku wanafunzi wakiwa ni 5,300 ambapo 4,888 wamekosa nafasi za bweni hasa
wanaotoka mikoani.
Nyingine ni uhaba wa wahadhiri wa masomo
ya Sayansi na wenye Shahada ya Udaktari wa Falsafa, miundombinu isiyo rafiki
kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, uchakavu wa miundombinu, ukosefu wa fedha
za maendeleo kutoka serikalini na ukosefu wa nyumba za kuishi wageni.
Katika kukabiliana na changamoto ya
mabweni, alimwomba Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Jakaya Kikwete
kukisaidia kupata maeneo Mkuranga na
Bagamoyo ili kujenga mabweni na kampasi.
Dk Kikwete aliwapongeza wahitimu hao na
kuwasihi watekeleze walichojifunza wakiwa chuoni.
0 comments:
Post a Comment