Mashaka Mgeta
Mashaka Mgeta |
ZIPO tuhuma nyingi zinazotolewa nchini
kuhusiana na matumizi mabaya madaraka, hujuma dhidi ya rasilimali za umma ama
aina nyingine za ufisadi.
Kuibuliwa kwa tuhuma hizo na nyingine
zinazofanana na hizo hakukuanza katika awamu ya tano chini ya Rais John
Magufuli, la hasha.
Tuhuma kama hizo na nyinginezo
zimekuwapo tangu wakati wa utawala wa awamu wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na marais waliomfuata, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na
Jakaya Kikwete.
Kila Rais katika utawala wake,
alizibaini tuhuma hizo na kuzishughulikia kwa namna yake, ile iliyotofautiana
kutoka awamu moja hadi nyingine.
Lakini ukweli ni kwamba tuhuma za
ufisadi zimekuwapo katika tawala zote na zikashughulikiwa kwa namna
zinazotofautiana.
Hata sasa wakati Rais Magufuli
akisadikiwa kuwa ‘mkali’ dhidi ya wanaohujumu rasilimali za umma ama kutumia
vibaya madaraka yao, wapo waliobainika kuwa kinyume na mwelekeo huo, wakajiweka
kando na azma njema ya kuondokana na uovu huo.
Ndio maana Rais Magufuli amejikuta mara
kadhaa akilazimika kutengua uteuzi wa viongozi aliowakuta ama aliowateuwa, ili
mradi tuhuma zinazotolewa dhidi yao hazikidhi vigezo na sifa za kiongozi
anayepaswa kuutumikia umma katika utawala wake.
Hivi karibuni, kumeibuliwa kashfa
inayolihusu Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), kuhusu ununuzi wa
ardhi ma ujenzi wa makazi katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Zipo taarifa zinazodai kuwa NSSF
ilinunua ekari 300 kwa kutoka kwa mbia mwenzake, kampuni ya Azimio Housing
Estates (AHEL) kwa zaidi ya Sh milioni 800 kwa ekari.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, NSSF
ikisaidikiwa kuwa miongoni mwa mashirika ya hifadhi yenye idadi kubwa ya
wanachama, inamiliki viwanja vingine katika eneo hilo vikiwa na thamani ya Sh
milioni 4.5 kwa ekari.
Lakini hata ujenzi wa makazi hayo
kupitia mradi wa mji wa kisasa, unatajwa kughubikwa na ufisadi wa mabilioni ya
Shilingi za kitanzania, hali inayoibua hoja za kuwapo uchunguzi wa kina na
kuchukua hatua dhidi ya wahusika.
Ni jambo lililo wazi kwamba NSSF ni
shirika la umma, raia wa Tanzania pasipo kujali itikadi, dini, kabila ama
tofauti yoyote, ni wanachama kwa mujibu wa sheria zinazowaongoza.
Hivyo kuyumbishwa ama kuhujumiwa kwa
NSSF kwa namna yoyote, maana yake ni kuyaathiri maslahi ya raia walio wengi,
hivyo kuwa na athari kwa jamii pana ya Watanzania.
Sasa zinapotokea tuhuma, bila kujali
ikiwa zimethibitishwa ama lah, zikaelekezwa kwa `shirika kubwa’ kama NSSF,
hakuna sababu ya wenye dhamana za kisiasa, kuiondoa jamii kutoka kwenye hoja ya
msingi na kujielekeza katika kukidhi matakwa binafsi ama ya chama cha siasa.
Kwa mfano, mwishoni mwa wiki iliyopita,
kuliibuka majibizano ya haja yanayoendelea kujadiliwa na watu, kati ya Msemaji
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher Ole Sendeka na chama cha ACT
Wazalendo kinachoongozwa na Zitto Kabwe.
Asili ya majibizano hayo ni hoja ya Ole
Sendeka kuhusu kumtilia shaka Zitto kwa kile anachokiita kuwa ni ‘kuishambulia’
Serikali ya Rais John Magufuli inayowajibika katika kuwashughulikia mafisadi.
Ole Sendeka akaenda mbele zaidi na
kupendekeza Serikali kupitia vyombo mahususi, kuchunguza mali na akaunti za
Zitto aliyekuwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Hata hivyo, chama cha ACT Wazalendo
kupitia kwa Habib Mchange, wakajibu hoja za Ole Sendeka, hivyo kuigeuza suala
la msingi katika kuutafuta ukweli kuhusu ufisadi unaotajwa NSSF, kuwa la
kisiasa.
Ninatambua uhuru wa kujieleza kwa kila
raia, kwamba linapotokea jambo kama kashfa dhidi ya NSSF, wapo watakaojenga
hoja tofauti, zile za kuuibua ukweli, kushawishi ama kujilinda dhidi ya tuhuma
husika.
Lakini uhuru huo haupaswi kuwa wenye
`kuiondoa mezani’ hoja mahususi ya vita dhidi ya ufisadi, ikafanywa kuwa
malumbano na ‘mipasho’ ya kisiasa isiyokuwa na tija.
Tatizo la kijamii, linalotokea kwenye
jamii na kuiathiri jamii husika, linapaswa kujadiliwa kwa msingi wa suala na si
kumlenga mtu binafsi ama kutafuta kuungwa mkono ili kuiokoa hadhi ya chama cha
siasa ama vinginevyo.
Jambo lililo wazi ni kwamba zipo tuhuma
zinazoelekezwa kwa NSSF, kwamba katika utendaji kazi wake, imefikia wakati
kukawapo mianya iliyotumika kufanya ufisadi unaoweza kuwaathiri wanachama na
taifa kwa ujumla wake.
Tatizo la kijamii kama tuhuma dhidi ya
ufisadi linapogeuzwa kuwa sehemu ya malumbano ya kisiasa, mwelekeo wa uliopo
unabadilishwa kiasi kwamba hata wahusika wanaweza kuutumia mwanya huo kufanikisha
nia ya kupotosha na kuuficha ukweli.
Kama wanasiasa wanakuwa sehemu ya jamii
inayoguswa na uovu kama unaodaiwa kutokea NSSF, iweje waanze ‘kutupiana
madongo’ badala ya kujielekeza katika suala linalohityaji ufumbuzi, nalo ni
ufisadi?
Bahati nzuri Zitto na Ole Sendeka
wamewahi kuwa wabunge, wakishiriki mijadala ikiwamo iliyowaunganisha wabunge
pasipo kujali tofauti zao, wakautetea umma dhidi ya uovu.
Vivyo hivyo inapaswa kuwa hata sasa,
wakati ambapo suala la msingi ni ufisadi unaodaiwa kufanyika NSSF, basi na iwe
hivyo, kwamba kinachopaswa kufanyika ni kushughulikia ufisadi na si
mashambulizi ya kisiasa dhidi ya mtu binafsi.
Mwisho
0754691540
0 comments:
Post a Comment