Suleiman Msuya
Profesa Ibrahim Lipumba |
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema dhambi
ya usaliti inamtesa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim
Lipumba.
Aidha, CUF imesema Lipumba amezoea na
ameshaonja ladha ya kutumika hali ambayo hawezi kuiacha kwani inamfaidisha.
Kauli hiyo ya CUF inakuja ikiwa ni siku
moja baada ya Lipumba kuibuka na kumjibu Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif
Hamad kwa kumtaka afuate taratibu ili kufanikisha mikutano yake.
Taarifa iliyotolewa na Ofisa Mawasiliano
na Uchaguzi CUF Taifa, Abdulrahman Lugone, ilisema kuwa kiongozi huyo amekuwa akikisaliti chama hicho kwa
muda mrefu ikiwamo, mwaka 2010 kwa kumsaidia mgombea wa Chama Cha Mapinduzi
Rais mstaafu Jakaya Kikwete kushinda.
“Mwaka 2015 alipoona hawezi kugombea
urais akajua wanunuzi wataona hana thamani, akaona njia ni kujitoa kwenye chama
ili wanachama wavurugike ambapo mpango wake ulifeli vibaya kwani CUF ni
taasisi,” alisema.
“Wanunuzi wake, CCM, waanze kutafuta
bidhaa nyingine kwa sababu CUF ilishamalizana naye. Waendelee kumpa ulinzi wa Polisi,
wampigie saluti, wampe uenyekiti wa chama kwa nguvu ya dola yote hayo
hayataihamisha CUF kwenye ajenda zake katika kuwapigania Watanzania na
Wazanzibari kwa ujumla,” alisema.
Lugone alisema ni vema jamii ikajiuliza
maswali ya msingi ni mahali gani duniani
kiongozi wa juu wa taasisi kubwa kama CUF ambaye aliwahi kuandika barua ya
kujiuzulu na kuiacha ofisi yake kwa muda wa miezi kumi akarudi kwa mfumo huo wa
Lipumba.
Alisema CUF ilichagua kiongozi mbadala
wa nafasi hiyo hiyo, hivyo wao hawapo tayari kuona utaratibu wa chama ukikiukwa
kwa maslahi ya mtu mmoja.
0 comments:
Post a Comment