Suleiman Msuya
Jaji Joseph Warioba |
WAZIRI Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba
ameombwa kubaki na msimamo wake wa kuikosoa Serikali inapokosea, licha ya kuteuliwa
na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Maombi hayo yalitolewa na watu wa kada mbalimbali
walipozungumza na JAMBO LEO wakisisitiza kwamba Warioba akibaki na msimamo wake
wa awali atakuwa ameonesha uzalendo.
Mwanaharakati Renatus Mkinga alisema
itakuwa ni jambo la aibu iwapo Warioba atabadilika kwa cheo hicho ambacho ni
cha kuteuliwa.
Alisema mtu anayejitambua hawezi
kubadilika kisa cheo, hivyo iwapo ataonesha dalili hizo atakuwa hatendei haki
wananchi.
“Mimi ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ila sijawahi kuonekana ni kitoka kwenye
msimamo wangu na pale ambapo Serikali inapatia nasifia, huo ndio msimamo unaotakiwa,”
alisema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF,
Julius Mtatiro alisema haamini kuwa Warioba anaweza kubadilishwa msimamo wake
kwa vyeo kwani ana uzoefu mkubwa katika uongozi.
Mtatiro alisema ipo dhana ya viongozi wa
Afrika kuwapa nafasi wakosoaji ili wasikosoe Serikali zao, hivyo kwa njia
nyingine inaweza kuwa ndilo lengo la Rais.
“Ni vigumu unapokuwa mteule wa Rais
uanze kukosoa Serikali yake hata mimi hapa yakinikuta hayo na nikikubali
nawajibika kufuata yale ambayo Serikali inafanya,” alisema.
Alisema kiujumla anaona Warioba ameingia
kwenye mtego hali ambayo itamshinda kuzungumzia Katiba na mambo mengine muhimu
kwa kukosoa.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (UDSM), Dk Onesmo Kyauke alisema kwa nafasi kama ya Warioba kuwa
mwoga katika yale ambayo unaamini ni kuondoa uzalendo wako.
“Iwapo angeteuliwa kuwa waziri, katibu
mkuu, mkuu wa mkoa au wilaya hayo ambayo yanatajwa kubadilisha msimamo
yangetokea ila kwa nafasi hiyo sioni uhusiano,” alisema.
Irene Joseph alisema kwa upande fulani
inaweza kuwa njia ya kufungwa midomo iwapo alikuwa anaiomba nafasi hiyo itokee.
Alisema Serikali ya sasa imeonesha
dalili za kuhangaika na watu ambao wanaikosoa hasa ambao wako kwenye mfumo,
hivyo inawezekana ni mipango ambayo imefanywa kumtuliza, kwani alionesha
msimamo katika baadhi ya mambo.
Meya wa Kinondoni na Diwani wa kata ya
Ubungo, Boniface Jacob alisema kimsingi Warioba alianza kuonesha mabadiliko wakati
wa uchaguzi kwa kupigia kampeni CCM, hivyo hana jipya katika kuikosoa Serikali.
Alisema Serikali imeshatambua kuwa watu
wengi wenye kuisema wanakabiliwa na njaa, hivyo njia mojawapo ya kuwafunga
midomo ni kuwapa nafasi na ndicho kinafanyika.
“Si kwamba nasema Warioba ana njaa,
lakini angalia wale CCM ambao walionekana kuwa na njaa wamepewa nafasi sitaki
kuwataja, naamini na wewe unawajua,” alisema.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar,
Salum Mwalimu alisema kwa mtazamo wake, Warioba anastahili nafasi aliyoteuliwa
na hana jipya ambalo anaweza kulizungumza likabadilisha msimamo wa Serikali.
Alitolea mfano Katiba iliyopendekezwa,
ilishapita katika mikono yake hivyo na sasa ni mamlaka nyingine inahusika
kuikamilisha jambo ambalo Warioba hawezi kubadilisha.
Mwalimu alisema iwapo misimamo aliyokuwa
anaisimamia ilikuwa ni ya kizalendo haiwezi kubadilika kwa kigezo cha kuteuliwa
kuwa Mkuu wa Chuo.
0 comments:
Post a Comment