Moses Ng’wat, Mbeya
Simbachawene |
OFISI ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imetangaza kuwachukulia hatua
kali mameya wa majiji, wenyeviti wa halmashauri za miji na wilaya, madiwani na
watendaji wa halmashauri nchini, watakaobainika kutumia magari ya halmashauri
kwa shughuli zao binafsi.
Pia, imewaonya
viongozi hao kuacha mara moja tabia iliyoibuka ya kuchagua ama kupendekeza
kuendeshwa na baadhi ya madereva wanaoweza kutekeleza matakwa yao na kuwakataa
madereva wanaosimamia taaluma zao na utumishi wa umma.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya, Ameichiory Biyengo
alibainisha hayo juzi alipokuwa akisoma waraka mahususi kutoka Tamisemi kuhusu
matumizi ya magari ya halmashauri wakati wa kikao cha baraza la madiwani.
“Maelekezo ya
barua hii yasomwe kwenye mabaraza ya madiwani kwa kuwa waheshimiwa
madiwani ndio wasimamizi wakuu wa mali za halmashauri ili wao wenyewe waongoze
katika utunzaji wa mali hizo na waweze kusimamia ipasavyo utekelezaji wa
maelekezo haya,” Biyengo alinukuu sehemu ya waraka huo.
Kwa mujibu wa waraka
huo, Tamisemi imechukua hatua hiyo baada ya kupokea maombi mbalimbali ya magari
kutoka kwa wakurugenzi wa halmashauri kufuatia kukabiliwa na upungufu wa vitendea
kazi kulikosababishwa na uchakavu wa magari na sababu nyingine.
“Pamoja na
maombi hayo, uchunguzi uliofanywa na ofisi hii, umebaini kuwa uchakavu wa
magari ya halmashauri unatokana na matumizi mabaya ya magari kwa viongozi wa
siasa na maofisa waliopewa dhamana ya kuyatumia magari hayo vibaya kwa shughuli
binafsi, ” ilinukuu sehemu ya waraka huo.
Katika waraka
huo wa Oktoba 12 mwaka huu na kusainiwa na katibu mkuu wa wizara hiyo, Mussa
Iyombe umewataka wakurugenzi wote wa halmashauri za majiji, miji na wilaya
kuusoma waraka huo kwenye vikao vya mabaraza ya madiwani kwa kuwa
wao ndio wenye dhamana ya kusimamia mali za halmashauri.
“Ipo tabia ya
baadhi ya viongozi wa kisiasa na watumishi wa Halmashauri kutumia magari ya halmashauri
kwa shughuli zao binafsi, hali hii inasababisha viongozi hao kuchagua ama
kupendekeza kuendeshwa na baadhi ya madereva ambao wanaweza kutekeleza matakwa
yao na kuwakataa madereva wanaosimamia taaluma zao na za utumishi wa umma.”
Waraka huo pia unaagiza
shughuli zote za upangaji wa magari kwa madereva katika halmashauri nchini
ufanyike kwa kuzingatia weledi wa taaluma na si upendeleo au maslahi
binafsi ya kiongozi husika .
Kutokana na hali
hiyo Tamisemi imesema haitasita kumchukulia hatua za kinidhamu na kisheria kiongozi
au mtumishi yeyote atakayebainika kukiuka kanuni, taratibu na maadili ya
utumishi wa umma kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13
ya mwaka 1995 na Sheria ya Utumishi wa Umma namba 8 ya mwaka 2002.
0 comments:
Post a Comment