Mohamed Mchengerwa |
MBUNGE wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa (CCM), amesema
atashughulika na ufisadi katika vikundi vya kuweka na kukopa vilivyopo katika
jimbo hilo ili kuhakikisha fedha zinazopatikana zinatumika kwa matumizi sahihi.
Mchengerwa aliyasema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa
vikoba endelevu ambavyo vimejumuisha vikundi tisa. Hadi sasa vikoba hivyo vina akiba
ya zaidi ya Shilingi milioni 45.
‘’Pamoja na jitihada hizi za kuhakikisha tunajikwamua na
umasikini kwa kujiunga katika vikundi ili tuweze kusaidiana kirahisi, bado kuna
watu ambao wanafanya ufisadi ili kuviua vikundi. Nitakwenda kushughulika nao
wote, ikiwa ni njia ya kumuunga mkono rais wetu John Magufuli ambaye kila
kukicha anapingana na mafisadi,’’ alisema.
Mchengerwa ambaye baada ya uzinduzi wa vikoba hivyo
alichangia shilingi 6,500,000 na kuahidi kutoa milioni mbili zingine, aliwataka
wanavikundi hivyo kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika katika maendeleo na
kuonya wenye mtindo wa kugawana fedha zinapotolewa.
‘’Naomba fedha hizi zitumike katika matumizi sahihi, nakumbuka
hivi karibuni nilitoa pikipiki katika vikundi, lakini taarifa zilizopo ni
kwamba watu wameenda kuuza na kugawana fedha jambo ambalo si sahihi. Tunajirudisha
nyuma wenyewe,’’ alisema Mchengerwa.
Alisema wananchi wa Rufiji ni maskini na wapo nyuma
kimaendeleo, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anakuwa mstari wa mbele
kuukataa umasikini huo kwa vitendo.
‘’Nimejitolea kusaidia watu wa Rufiji kwa kuwa
mlinichagua ili niwawakilishe. Naombeni kila mmoja aguswe na umaskini tulionao
na awe na dhamira ya dhati ya kuutokomeza.”
Aliendelea “Vikundi hivyo vitumike vizuri mkopeshane ili muweze
kuendesha na kuanzisha biashara zenu. Naahidi kuwa bega kwa bega na nyie na leo
hii (juzi) nawakabidhi mke wangu Farida Mchengerwa kuwa mlezi wenu ili
msaidiane naye,’’alisema.
Akizungumza katika tukio hilo Farida aliwataka wananchi
kutumia fursa hiyo kujiunga na vikundi hivyo ili waweze kukopesheka, kwani
inajulikana kuwa maskini hakopesheki kutokana na masharti yanayowekwa na
taasisi za fedha.
Akizungumza kwa niaba ya wanavikundi wenzake, Abdulrahman
Hafidh, alisema vikundi hivyo kwa sasa vina wanachama zaidi ya 220.
Alitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na
uelewa mdogo wa wanavikundi kuhusu vikoba endelevu.
0 comments:
Post a Comment