‘Wauaji’ kada wa Chadema wagoma


Salum Maige, Geita


Alphonce Mawazo
MAHABUSU wanne kati ya 11 wanaokabiliwa na kesi ya mauaji  ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa, Alphonce Mawazo, wamegoma kuingia mahakamani.

Badala yake wamekatalia katikati ya barabara ya lami wakishinikiza wahusika wakamatwe ili wao waachwe huru.

Mahabusu hao waligoma jana kwa walichodai ni kubambikiwa kesi hiyo ilhali wahusika wanafahamika kwa majina na vyeo vyao.

Washitakiwa ambao majina yao hayakufahamika mara moja kutokana na polisi kuimarisha ulinzi eneo hilo wakizuia waandishi wa habari kuwahoji na kuwapiga picha, walizua kizazaa hicho kuanzia saa mbili hadi saa tatu asubuhi wakiwa wamekaa barabarani.

Walitolewa Gereza Kuu la Wilaya ya Geita, wakipelekwa Mahakama ya Wilaya kwa kutajiwa kesi yao.

Katika kesi hiyo, watuhumiwa ni 11 ambao ni Alfan Kyalubota, Epafula Mapinda, Hashimu Omary, Elias Sadick, Habibu Issa na Kalulinda Bwire.

Wengine ni Phinias Andrea, Deus Elias ‘Pozi la Yai’, John Innocent ‘Tetes’, Robert Miano na mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Majaliwa.

Wote wanatuhumiwa kumuua Mawazo Novemba 14, mwaka jana katika kijiji cha Ludete kwenye mji mdogo wa Katoro wilayani Geita.

Walipofika katikati ya barabara, kabla ya kuvuka ili waingie kwenye viwanja vya Mahakama hiyo, walijigawa makundi mawili na wanne wakagoma na kukaa chini katikati ya barabara hiyo, huku wengine wakienda mahakamani.

Wananchi waliokuwa kwenye viwanja vya Mahakama na wapitanjia waliachwa midomo wazi na hali ya mshangao, na kusogea walikokuwa wamekaa mahabusu hao kwa ajili ya kushangaa tukio hilo na kusababisha umati mkubwa wa watu eneo la tukio, wakati huo mahabusu hao walikuwa wakipiga kelele kwa kupaza sauti kudai haki itendeke kwenye suala hilo.

Wakiwa wamekaa katikati ya barabara ya Lami, huku wakiwa chini ya ulinzi wa polisi, mmoja wao alisikika akisema: ‘’Haiwezekani, tunaendelea kusota gerezani wakati watuhumiwa wanafahamika kwa vyeo na majina na wengine wanakuja kutusanifu gerezani, wakiwa wamevalia suti lakini hawakamatwi…Mkuu wa Gereza anajua na polisi wanawajua, lakini hatuoni wakikamatwa.

‘’Tumechoka, tunamwomba Mkuu wa Wilaya au wa Mkoa waje hapa tuwaeleze wahusika ni akina nani ili wakamatwe na sisi tuachwe huru…haiwezekani tukaendelea kukaa gerezani wakati Mkuu wa Gereza na Polisi tulishawaambia wahusika ni akina nani.

“Lakini hatuoni dalili za kuwakamata…tuko tayari kurudi gerezani, lakini hatutaki kwenda mahakamani, tukafanye nini na kesi zetu hazisikilizwi?’’ Alihoji mmoja wa mahabusu hao kwa uchungu na kuacha mshangao kwa watu waliokuwa wamejaa eneo hilo wakishangaa tukio.

‘’Polisi wanajua kabisa hii kesi haituhusu sisi lakini haikamatwi na wahusika wengine tunao kwenye kesi hii ndiyo maana wanakuja mahakamani wamevaa fulana zimeandikwa ‘Hapa Kazi Tu’…tunawaomba viongozi waje hapa watusikilize, ndiyo tutakubali kuingia mahakamani vinginevyo hatuendi kama kutuua watuue tu, tumechoka,’’ alisikika mahabusu mwingine akilalamika kwa sauti.

Wakati wakipaza sauti kutoa kilio chao saa 3 asubuhi, mwanamke mmoja ambaye hakufahamika jina lake mara moja, aliyekuwa akirekodi sauti za mahabusu hao na kupiga picha alifuatwa alipokuwa na polisi kisha kunyang’anywa simu na kuamriwa kutoweka eneo hilo mara moja ambapo alifanya hivyo, huku akiacha simu yake kwa askari hao na haijafahamika iwapo ataifuatilia au la.

Baada ya muda, walifika Mkuu wa Kituo cha Polisi Geita, Julius Masanyiwa na maofisa usalama na kuwahoji kuhusu madai yao, lakini mahabusu hao waligoma kutoa maelezo wakishinikiza kuwa wa kuwapa maelezo yao ni viongozi wa Serikali, vinginevyo warejeshwe gerezani na si mahakamani.

‘’Tumesema tunataka kuzungumza na Mkuu wa Mkoa au wa Wilaya, si ninyi maana malalamiko yetu mnayajua lakini hamtaki kukamata wahusika…sasa tutoe maelezo ili iweje?’’ Alihoji mmoja wa mahabusu hao.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Kituo na wenzake waliwaacha kwa muda   na kutoka eneo hilo na waliporejea walikubaliana na matakwa ya mahabusu hao ya kuwarudisha gerezani wakakubali. 

‘’Kama ni gerezani twendeni, lakini si mahakamani maana viongozi tuliotaka waje hapa hawajafika gerezani, twendeni wala hakuna shida,’’ walisikika mahabusu hao huku wakinyanyuka eneo hilo na kuelekea gerezani.

Mawazo (39) aliuawa kwa kushambuliwa kwa silaha za jadi na watu wasiojulikana kando ya barabara kuu mtaa wa Ludete, Katoro wilayani Geita siku chache baada ya uchaguzi mkuu kufanyika ambapo alikuwa mgombea wa CHADEMA jimboni Busanda.


Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo