MAMA mzazi wa Antonia Msoka (17) anayeongezeka uzito wa kilo
mbili kila mwezi amewaomba msaada Watanzania wamsaidie ili mwanawe atibiwe na
kurudi katika hali yake ya kawaida.
Solome Kisusi mkazi wa wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, akizungumza
jana kwnye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) walikolazwa, alisema tatizo la
mwanawe lilianza akiwa mdogo.
Alisema alizaliwa alowa na uzito wa kilo 2.3 na baada ya
mwezi aliongezeka kilo moja.
"Alizaliwa akiwa na kilo 2.3, baada ya mwezi
akaongezeka kilo moja, lakini baada ya hapo kila mwezi akawa anaongezeka kilo mbili,"
alisema Salome.
Aidha, alisema baada ya kufikisha miezi saba alikuwa
tayari na kilo 18, kutokana na hali hiyo kutokuwa ya kawaida walimpeleka hospitali
ya wilaya ya Geita ambako waliambiwa hawana uwezo wa kubaini tatizo na kuambiwa
waende Bugando, Mwanza.
Salome alifafanua kuwa baada ya kufika Bugando,
walifanyiwa vipimo na vyote vikaonesha
hana tatizo hivyo kushauriwa waende Muhimbili ambako walifanyiwa vipimo na bado
hakuonekana na tatizo.
Hivyo, alisema kutokana na hali hiyo waliambiwa warudi
waangalie akifikisha miaka mitatu bila kutembea wamrudishe, lakini alitembea
hivyo kutokana na hali ya kiuchumi hawakurudi na hawakuwa na hofu sana kwa kuwa
mtoto alikuwa anatembea.
Aliongeza kuwa baada ya Antonia kufikisha miaka 12 hali
ilibadilika akashindwa kutembea, akawa
anatembea kwa magoti huku akilalamika kuumwa tumbo na miguu kuwaka moto.
Alieleza, kwamba hali hiyo ilipotokea, mwaka jana
wakarudi Bugando kufanyiwa vipimo viwili kati ya vitatu alivyoainishiwa ambavyo
mmeng'enyo wa chakula na sukari, vyote havikuwa na shida na kilichobaki kilikuwa
cha homoni.
Alisema waliambiwa warudi Muhimbili kwa vipimo zaidi
ambapo alibainisha kuwa inaonekana kuwa vipimo na matibabu zaidi yatafanyika
nje, hivyo akaomba msaada kwa wananchi wamchangie ili kufanikisha matibabu ya
mwanawe.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, Kisukari na Magonjwa
ya Homoni wa MNH, Dk Wolfgang Benard alisema Antonia kwa takribani wiki tatu
yuko Muhimbili kwa tatizo lake la kuongezeka uzito kwa kiasi kisicho cha kawaida.
"Uzito huo umekuwa ukiongezeka kila mwezi au kila mwaka na hadi sasa kulingana na uzito alionao kuwa mkubwa, hawezi kutembea kutokana na miguu kushindwa kuhimili uzito wa mwili," alisema Dk. Benard.
Alisema kutokana na kutobaini tatizo, waliamua aletwe Muhimbili ambako walifanya vipimo na vimeendelea kutoonesha kuwa na tatizo lolote.
Alifafanua kuwa tatizo la Antonia halisababishwi na homoni kwa sababu wengi wenye tatizo la namna hiyo chanzo huwa ni homoni ambapo alisema baada ya vipimo hakukuwa na shida ya homoni.
Aidha, alisema wanaona tatizo lake ni jeni ambayo matibabu
yake ni upasuaji ambao umekuwa ukifanyika sana nchi za nje na kwamba wagonjwa
wanaofanyiwa hivyo hupoteza takribani uzito kwa asilimia 75.
Alisema kwa kuwa Antonia ana uzito wa zaidi ya kilo 150 atakapopasuliwa
baada ya miezi mitatu na minne atarudi kwenye kilo kati ya 70 na 80.
Alisema wanaamini baada ya kupungua atatembea tena lakini
hakuna uhakika huo kwa kuwa hajatembea kwa muda mrefu, hivyo haiwezi kujulikana
miguu itakuwa imeathirika kwa kiasi gani.
Dk Benard alifafanua kuwa kwa sasa wapo katika hatua za
mwisho ili kuhakikisha antonio anapelekwa nje kufanyiwa upasuaji.
0 comments:
Post a Comment