Hussein Ndubikile
Ummy Mwalimu |
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa onyo kwa vituo vinavyotoa chanjo
ya homa ya manjano bila vibali kuacha mara moja kabla havijachukuliwa hatua za
kisheria.
Aidha, imewahadharisha watu wanaochapisha,
kusambaza na kuuza vyeti vya chanjo hiyo, kwani hatua za kisheria zitachukuliwa
dhidi yao.
Hatua hiyo imekuja baada ya kubainika
kuwapo vituo visivyo na vibali vinavyotoa chanjo ya ugonjwa bila ruhusa ya
wizara hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa vyeti na mihuri mipya ya chanjo ya ugonjwa
huo, Waziri alisema wizara imeshapata
taarifa ya vituo vinavyoendesha huduma hiyo bila vibali, hali inayohatarisha
maisha ya wagonjwa huku akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kukiuka taratibu na
sheria za utoaji chanjo hiyo.
“Wizara inatoa onyo kwa vituo
vinavyoendelea kutoa chanjo bila vibali viache na wale wanaovichapisha na kuvisambaza waache,
tutawachukulia hatua kali kisheria,” alisema.
Alisema tangu ugonjwa huo uripotiwe Desemba
mwaka jana iliripotiwa kuwa idadi ya wagonjwa wa homa hiyo nchini Angola ni
takribani watu 4,347 huku 377
wakiripotiwa kupoteza maisha na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wagonjwa
walikuwa 2,987 waliofariki dunia ni 121.
Alisisitiza kuwa makundi ambayo yamo
katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo ni wasafiri, watu wanaojihusisha na
shughuli za kitalii na uwindaji pamoja na wafanyakazi wa viwanja vya ndege.
Aliongeza kuwa gharama za huduma za
chanjo ya homa ya manjano ni Sh 20,000 kwa raia za watanzania na dola 50 kwa
raia wa kigeni.
Waziri Ummy alisema chanjo hiyo
itatolewa katika vilivyoko viwanja vya ndege vya Julius Nyerere, Kilimanjaro,
Mwanza, Bandari ya Dar es Salaam, Tanga, Mwanza na Kigoma na Kituo cha Afya cha
Mnazi Mmoja.
Vingine ni mipakani Horohoro, Namanga,
Holili, Tarakea, Sirari, Isaka, Mutukula, Mtambaswala, Kasumulu na Tunduma.
Pia alisema utoaji chanjo hiyo unakabiliwa
na changamoto ya kuwapo baadhi ya
wananchi wasiokuwa waaminifu maarufu kama vishoka ambao hughushi vyeti vya
chanjo na kuwapa wasafiri pasipo kuchanja.
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa
Muhammad Kambi alisema ugonjwa huo bado haujaingia nchini, tangu ulipotokea
mwaka 1960 huku akiongeza upo nchi jirani za Kenya, DR-Congo na Angola.
Katika hatua nyingine, Serikali
imesajili waganga wa tiba asili na tiba mbadala 14,000 na vituo vya 180.
0 comments:
Post a Comment