Polisi: Siasa inatukwamisha


*Kamanda Sirro asema uvumi, kutotoa ushahidi ni vikwazo
*Ataja uadilifu kama siri ya mafanikio ndani ya Jeshi lake



Fidelis Butahe

Kamanda Simon Sirro
KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, ametaja mambo matatu ikiwamo siasa kuwa yanakwamisha jitihada zao.

“Kuna tofauti kubwa kati ya siasa na masuala ya ulinzi na usalama, watu wasichanganye haya,” amesema Kamanda Sirro kwenye mahojiano maalumu juzi na gaeti hili.

Hata hivyo, alisema Jeshi lake linafanya juhudi kubwa kukabiliana na   uhalifu Dar es Salaam.

Kamanda Sirro alisema haipaswi watu kuchanganya siasa na utendaji kazi wa Jeshi hilo.

Sirro alitoa kauli hiyo huku kukiwa na mvutano na mkanganyiko kati ya Jeshi hilo na baadhi ya vyama vya siasa, kuhusu kuzuiwa na kuruhusiwa kufanya mikutano ya kisiasa.

Kamanda aliyepokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake, Suleiman Kova aliyestaafu hivi karibuni, alitaja mambo mengine mawili yanayokwamisha Polisi kuwa ni uzushi juu ya uporaji unaodaiwa kufanywa na vikundi na wananchi kushindwa kutoa ushahidi mahakamani dhidi ya wahalifu.

“Wapo wanaohusisha ulinzi na usalama na mambo ya siasa. Yaani utakuwa ukizungumzia suala la vikundi vya ulinzi  shirikishi wao (wananchi) wanapinga na kudai haiwahusu kwa kuwa ni wanachama wa chama fulani,” alisema.

“Katika uhalifu hakuna anayeulizwa ‘wewe ni wa chama gani’.  Siasa ibaki siasa na usalama uwe usalama. Ulinzi na usalama ni jambo la kila mtu.  Siasa itumike kulinda na kuleta amani na utulivu na si kuharibu amani na utulivu,” alisisitiza.

Katika suala hilo hilo la siasa, Kamanda Sirro aliulizwa juu ya tuhuma zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kudai alipokea rushwa ya Sh milioni 50 kutoka kwa kikundi cha wafanyabiashara 10 wa shisha, ili waendelee na biashara hiyo, ambapo alionesha kushangazwa.

Kamanda huyo alisema: “Sina jibu kuhusu shisha. Ila tunaendelea kukamata wafanyabiashara wa shisha.

“Nimezunguka sana hii Dar es Salaam. Nikiwa na nyota moja nilikuwa Oysterbay, baadaye nikaenda kuwa CID (Ofisa Upelelezi Makosa ya Jinai Wilaya) Kawe na baadaye Wazo, nimekuwa OCS Kijitonyama mpaka Mkuu wa Upelelezi Msaidizi wakati wa Gewe (Alfred-Kamanda wa Polisi Dar), kisha nikaenda Chang’ombe, lakini sikuwahi kusikia shisha,” alisema.

Alisema licha ya kuelezwa kuhusu shisha aliahidi kupambana na wahusika huku akikiri wazi kuwa hakuwa akijua kilevi hicho na kubainisha kuwa huenda kimeibuka nchini miaka ya hivi karibuni.

“Hata makamanda wenzangu waliopita sidhani kama walikuwa wanaijua shisha. Inaonekana ipo kwenye hoteli kubwa,” alisema.

Hata hivyo, alisema kwa amri iliyotolewa na Makonda ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na ni bosi wake, lazima operesheni hiyo ifanyike na wahusika wakamatwe.

“Mfano mpaka sasa tumeshawakamata watu watatu na baadhi ya mitambo yao na tutaipeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kuona madhara yake halafu baadaye watapelekwa mahakamani,” alisema.

Aliongeza: “Mkuu wa Mkoa amenielekeza na amekuwa ananielekeza kukamata shisha na makosa mengine kwa kuwa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama. Ninafanya hivyo kwa moyo mkunjufu.”

Alisema baada ya kuibuka matukio ya makundi ya vijana wadogo, kama Panya Road, Mbwa Mwitu na Watoto wa Mbwa, wakati mwingine kunaibuka uvumi mitaani juu ya makundi hayo kuvamia mtaa akisema:
 “Wakati mwingine tunafuatilia na kubaini kuwa ni uzushi tu.”

Alitaja kikwazo kingine kuwa ni wananchi kusita kutoa ushahidi mahakamani, jambo linalosababisha watuhumiwa kuachwa huru na kurejea tena mitaani.

“Kwenye uhalifu hasa wa makosa ya kubaka, hatupati mafanikio maana wananchi hawatoi ushahidi na hata wazazi nao wakati mwingine si wafuatiliaji sana. Unapotoa ushahidi mtu akafungwa miaka 30 mpaka atoke atakuonea wapi?” Alihoji.

Akizungumzia usalama Dar es Salaam, Kamanda Sirro alisema Polisi imedhibiti kwa kiasi kikubwa uporaji fedha kwa wananchi wanaotoka benki, uvamizi katika vituo vya Polisi, dawa za kulevya na kudhibiti vikundi vya uhalifu.

Sirro alisema tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo Februari 15, amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti waliokuwa wakitikisa Jiji huku akitaja mambo saba yaliyosaidia kupunguza uhalifu.

Alisema mafanikio ya Jeshi hilo kwanza yalitokana na nidhamu ya askari wake, akibainisha kuwa ndicho chanzo cha Polisi kukusanya Sh milioni 95 kutokana na makosa ya barabarani kwa siku.

“Mfano askari wa kikosi cha usalama barabarani waliokwenda kinyume na maadili tuliwaondoa. Askari wenye tuhuma ambazo hazina ushahidi tumewahamisha. Pia tuna kamati ya maadili ambayo hufuatilia utendaji wa kila askari,” alisema.

Alisema mambo mengine ni wananchi kutambua umuhimu wa ulinzi shirikishi, kukamatwa kwa silaha akitolea mfano silaha 25 zilizokamatwa hivi karibuni katika tukio la polisi kurushiana risasi na majambazi na kusababisha kifo cha askari mmoja.

“Majambazi wengi wamekamatwa na wengine kuuawa. Tumeimarisha vikosi vyetu vya kupambana na ujambazi na wizi wa magari. Hivi sasa ukiiba gari hufiki mbali utakamatwa tu,” alisema.

Alizungumzia kuibuka kwa matukio ya watoto wadogo kufundishwa mbinu za uhalifu, Sirro alisema lengo ni wanaowafundisha kuwatumia kujipatia kipato.

“Wakati mwingine utakuta mzazi ni mhalifu na anamfundisha mtoto mbinu. Tunapowabaini wazazi tunawachukulia hatua, ila watoto wapo wanaoweza kupelekwa kwenye mahakama za watoto na vituo vya ushauri nasaha,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo