Charles James
IKIWA ni mwaka mmoja tangu kuteuliwa kwa Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa, kushika wadhifa huo nchini, wasomi na wananchi wamejitokeza
kuelezea utendaji wake, huku wakimsifu kwa kuonesha mfano wa kuhamia Dodoma
ikiwa ni ahadi ya Serikali ya kuhamia mkoani humo.
Ahadi hiyo ya kuhamia Dodoma ilitolewa na Rais John
Magufuli mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM wakati akitoa shukrani zake za
kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho, Julai 23.
Baada ya kauli hiyo ya Rais, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
aliahidi kutimiza ahadi hiyo ili kuenenda na azimio lililofanyika miaka 43 la
kubadili makao makuu ya nchi kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na JAMBO LEO, wasomi na
wananchi walimwelezea Majaliwa kama mtu makini ambaye amekuwa akifanya kazi
bila kufuata vyombo vya habari, ambapo pia amekuwa mkweli katika kutimiza ahadi
anazotoa pamoja na kujali maslahi ya nchi.
Mhadhiri Msaidizi wa Sayansi ya Siasa na Utawala Bora
kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alisema hakuna mtu
aliyetegemea jina la Majaliwa kutangazwa kuwa Waziri Mkuu kutokana na kukosa
jina kubwa lakini utendaji wake umeonesha ni jinsi gani Rais hakukosea kumteua,
kwani amekuwa akifanya kazi kwa uwazi huku akionesha busara ya uongozi.
Mbunda alisema baada ya Rais kuahidi kuipeleka Serikali
Dodoma kabla ya mwaka 2020 hakuna mwananchi aliyetegemea, ingewezekana kutokana
na ahadi hiyo kutolewa kwa miaka 43, lakini Waziri Mkuu Majaliwa alionesha kuwa
inawezekana baada ya kuwa mtu wa kwanza kuhamia mkoani humo.
“Ni wazi kuwa Majaliwa anafanya kazi kubwa sana kwa kweli
ingawa hatuwezi kusema kwamba hana upungufu, lakini ameonesha mwanga hasa
katika kuhamia Dodoma, kwani amekuwa mstari wa mbele, lakini pia si mtu wa
kufanya kazi kwa kuonekana kama mawaziri wengine,” alisema.
Mbarouk Mchopanga ambaye ni mwananchi wa kawaida, alisema
Waziri Mkuu ameonesha kusimama kidedea katika kuhamia Dodoma, kwani aliahidi
kuhamia Septemba na kweli ametimiza ahadi hiyo, huku akimtaka kushughulikia
zaidi miundombinu ya mkoa huo, ili uweze kuendana na hadhi ya makao makuu ya nchi.
“Ni kweli ametimiza ahadi yake ya kuhamia Dodoma, lakini
ni wazi anapaswa pia kuhakikisha miundombinu ya mkoa huo inaboreshwa ili kuendana
na hadhi ya makao makuu ya nchi,” alisema.
Msomi mwingine ni kada wa CHADEMA, Profesa Mwesiga Baregu
alisema bado hajaona msingi wa kazi ya Waziri Mkuu, kutokana na kutoonekana
anasimamia nini hasa baada ya TAMISEMI kuondolewa chini ya ofisi yake.
Alisema Majaliwa amekuwa akifanya kazi chini ya kivuli
cha Rais kutokana na utendaji wake kutoonekana huku akisema kuhamia kwake
Dodoma huku miundombinu ya mkoa huo ikiwa mibovu, bado si jambo la kumpongeza,
ila akamsifu kwa kuonekana kwake Kagera wakati maafa ya tetemeko yalipotokea.
0 comments:
Post a Comment