Mary Mtuka
Dk. Hamisi Kigwangala |
OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) na ya Mtakwimu Mkuu wa
Serikali zimetakiwa kuhakikisha zinatumia teknolojia za kisasa za ukusanyaji takwimu
badala ya kutumia karatasi.
Mwito huo ulitolewa Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangala kwa
niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kwenye maadhimisho ya
Siku ya Takwimu Afrika ambayo hufanyika kila Novemba 18.
Alisema matumizi ya teknolojia yataipunguzia Serikali
gharama na mzigo wa kudurufu madodoso na kusafirisha mikoani na kuchapishwa
makala.
"Kutumika kwa teknolojia kutaendelea kuongeza ubora
wa takwimu zote zinazohitajika kupanga mipango ya maendeleo ya wananchi kwa
kuwa hupunguza makosa ya kibinadamu kwa kiasi kikubwa," alisema Dk
Kigwangala.
Alisema umuhimu wa kuboresha na kuimarisha takwimu za
uchumi na zenye ubora kwa utangamano wa kikanda Afrika utasaidia kuleta
mabadiliko ya kiuchumi na kufanikisha malengo 17 ya maendeleo pamoja na shabaha
zake 169 na viashiria 230.
Hata hivyo, alisema ni vema wakahakikisha kuwa wadau
kwenye mfumo wa utaoji na utumiaji takwimu wanaungana nao ili kupunguza mitiririko
isiyo sahihi ya takwimu.
Mkurugenzi Mkuu wa Takwimu, Dk Albina Chuwa alisema nchi
yoyote duniani yenye maendeleo au mabadiliko ya kiuchumi hupimwa kwa takwimu
rasmi, kwani wataalamu wa uchumi wanasema ukiboresha takwimu za uchumi
umeboresha uchumi wa nchi.
Alisema kaulimbiu ya mwaka huu kwenye maadhimisho hayo
iliyotolewa na Jumuia ya Afrika Mashariki
kwa kushirikiana na Ofisi ya Takwimu Afrika ambayo ni ‘Kuimarisha Takwimu za
Kiuchumi kwa Mtangamano wa Kikanda, Mabadiliko ya Miundo na Maendeleo Endelevu',
ililenga ukusanyaji na usambazaji wa takwimu za uchumi.
0 comments:
Post a Comment