*Vyakamatwa kambini vikijifunza karate, silaha
*Kamoja
kamwambia Sirro kanavyodhibiti adui
Emeresiana Athanas
JESHI la Polisi Kanda Maalumu, Dar es
Salaam linashikilia watoto wanne na wanawake wanne waliofichwa katika kambi
maalumu kwenye pori la Vikindu, Mkuranga mkoani Pwani, wakifunzwa mambo ya dini
na harakati za kigaidi ikiwamo kudhibiti maadui.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kamanda
wa Polisi wa Kanda hiyo, Simon Sirro
alisema watu hao (majina yamehifadhiwa), walikamatwa kutokana na operesheni
iliyofanyika kwenye pori hilo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Shabani
Maleck ambaye watoto wake wanne walitoroshwa.
Alisema kati ya watoto hao wenye umri wa
chini ya miaka minane, mmoja ni wa Maleck kati ya watoto wake wanne waliopotea,
huku wengine wakiwa hawajulikani wanakotoka.
"Baada ya mahojiano, imedhihirika
kuwa wengi waliachishwa shule na kuingizwa kwenye madrasa ambazo ndizo kambi
ambako wamekuwa wakijifunza ukakamavu, karate, judo, kutumia silaha na kudhibiti
maadui huku wakifundishwa kuwa polisi ndio maadui zao wakuu," alisema.
Alisema Jeshi hilo linaendelea na
upelelezi ili kubaini mtandao mzima katika suala hili, ili kutokomeza tabia ya
kuingiza watoto kwenye tabia ya uhalifu.
Kamanda Sirro alisema alipohoji mmoja,
alimwambia wamefundishwa jinsi ya kumpiga adui pigo moja shingoni na
kumdhibiti.
Alisema inaonekana baadhi ya watoto
wanaoripotiwa kupotea majumbani wamekuwa wakipelekwa maeneo kama hayo na
kufundishwa ugaidi.
Akizungumzia hatua hiyo, mzazi wa watoto
waliokamatwa katika kambi hiyo, Maleck alisema watoto wake walipotea tangu Juni
baada ya kutoroshwa na mama yao aliyetajwa kuwa ni Salma Mohamed.
"Walitoroshwa na mama yao na hadi
sasa pamoja na juhudi za Polisi tumefanikiwa kupata mmoja ambaye alikuwa kwenye
kambi hiyo," alisema.
Aidha, Jeshi hilo linashikilia watu
wanne kwa kujihusisha na wizi wa magari akiwamo Padri wa Kanisa Katoliki la
Sumbawanga, Demestrious Apolinary kwa kukutwa na gari la wizi aina ya Toyota
Land Cruiser namba T616 DCH mali ya Joseph Kayawaya.
Watu hao walikamatwa baada ya oparesheni
ya kikosi maalumu cha kuzuia wizi wa magari.
0 comments:
Post a Comment