Mwandishi Wetu
Samia Suluhu Hassan |
MAKAMU wa Rais,
Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imepiga hatua kulinda na kutetea haki za
binadamu kwa kuzingatia maazimio ya ndani na ya kimataifa ikiwamo haki ya
kuishi.
Samia alisema
hayo jana jijini Arusha wakati akifungua mkutano wa masuala ya demokrasia na haki za binadamu ya
Mahakama ya Afrika ya Watu na Haki za binadamu kwa niaba ya Rais John Magufuli.
Alisema Tanzania
ni mfano wa kuigwa Afrika kwa kuzingatia na kutekeleza ipasavyo mikataba ya
kimataifa inayolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za msingi
ikiwamo ya afya na elimu bila kubaguliwa.
“Serikali
itaendelea kutekeleza na kuzingatia matamko ya dunia yanayolenga kuhakikisha
wananchi wanapata huduma bora za kijamii ikiwamo haki ya kuishi,” alisema Samia.
Alisema anafurahishwa
na hatua zinazochukuliwa na baadhi ya nchi za Afrika kulinda na kutetea haki za
binadamu hasa za wanawake akiongeza kuwa bado kuna umuhimu kwa nchi zinazosuasua
kutekeleza mikataba hiyo, kuanza kuitekeleza ili kuhakikisha wanawake na watoto
wanapata haki sawa katika jamii.
Alibainisha,
kwamba Tanzania imepiga hatua kuingiza wanawake kwenye ngazi za uamuzi na kwa
sasa mpango kabambe unaandaliwa kuhakikisha sekta binafsi yenye idadi ndogo ya
wanawake kwenye ngazi za muamuzi kufanya hivyo.
“Utafiti
uliofanyika nchini unaonesha kuwa wanawake wengi walioingizwa kwenye bodi, zimeongeza
ufanisi wa kazi maradufu,” alisema.
Rais wa Mahakama
hiyo, Jaji Sylvain Ore alisema mkutano huo ni muhimu kwani unalenga kujadili na
kuweka mikakati kuhakikisha nchi za Afrika zinazingatia na kulinda haki za binadamu
hasa za wanawake.
0 comments:
Post a Comment