Omary Said, Kibaha
Akizungumza katika mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria
(OUT), kwenye kijiji cha Bungo kata ya Mkuza Kibaha Mjini jana, Rais Magufuli
alisema fedha hizo ziliwekwa kwenye benki hizo kwa lengo la kuzikopeshwa tena
kwa Serikali ili zilipiwe riba.
"Baada ya kubaini fedha hizo, tumezirudisha na Bodi
husika nimeivunja. Hiyo ndiyo changamoto ambayo Serikali yenu tunapambana nayo.
Imani yangu ni kwamba wahitimu, kwa kuwa mnatokea katika nafasi mbalimbali za
utumishi wa Serikali, mkitoka hapa mkatusaidie kuwatumikia wananchi ili
kuwaondolea changamoto zinazowakabili hatimaye wawe na imani na Serikali iliyoko
madarakani," alisema Rais.
Alieleza, kwamba kuna baadhi ya benki zimekuwa zikitumika
vibaya kwa kukopesha Serikali fedha zake zenyewe, badala ya kukopesha wananchi
na kwamba mambo hayo hukwamisha miradi ya maendeleo.
“Nitaendelea kufanya kazi kwa ufanisi bila kujali itikadi
za rangi, dini wala elimu. Nawatumikia wananchi wa hali ya chini, lakini naendelea
kuwaomba Watanzania muiunge mkono Serikali katika kuhakikisha wananchi wa hali
ya chini wananufaika na rasilimali zilizopo,” alisema Rais Magufuli.
Hivi karibuni, Rais Magufuli alitangaza kumwondoa Mwenyekiti
wa Bodi ya TRA na kuivunja Bodi hiyo katika hatua ambayo haikueleza sababu.
Kuhusu elimu, Rais Magufuli alisema Serikali itaendelea
kuboresha sekta ya hiyo, ili iwe ya kiwango cha juu na kwamba katika hilo,
hakutakuwa na mjadala, kwani lengo ni kuhakikisha kila mwanafunzi anayehitimu anakuwa
na sifa stahiki.
Alisema katika kuhakikisha hilo alipoingia madarakani,
alianza na mchakato wa utoaji elimu bure kuanzia ya msingi mpaka vyuo, jambo
ambalo pamoja na juhudi hizo, limekumbana na changamoto za hapa na pale
zilizosababishwa na baadhi ya watumishi wasio waadilifu, ambao walikuwa
wanaongeza idadi ya wanafunzi hewa.
"Kazi ya kutoa elimu bure ina changamoto zake, ndiyo
maana wakati Waziri mwenye dhamana, Profesa Joyce Ndalichako ulipokuwa
unazungumzia suala hilo, nami nilikuwa na yangu ya kuzungumza:
“Tangu nilipoingia madarakani na kuanza kutangaza elimu
bure kukawa na ongezeko kubwa la wanafunzi hewa, kazi hiyo ililazimika kuwepo
upungufu mkubwa wa madawati kazi ambayo kwa asilimia kubwa imefanikiwa, ingawa
kuna mikoa michache inaendelea kukamilisha," alisema Dk Magufuli.
Awali, akitoa taarifa ya Chuo, Mwenyekiti wa Baraza la
Chuo Kikuu Tanzania, Profesa Samwel Wangwe aliainisha changamoto kadhaa
zinazowakabili katika utekelezaji wake wa majukumu yakiwamo ya watu kutotambua
maana ya chuo hicho, ambacho malengo yake ni utoaji elimu bila kujali elimu ya
mwanafunzi anayehitaji kupata elimu kwenye chuo hicho.
"Chuo hiki kinatoa elimu na leo haya ni mahafali ya 10
ya Chuo hapa makao makuu ya Bungo, madhumuni ni kuwajulisha watu hapa kwamba
hapa ndipo kitovu cha Chuo, Kibaha tunatoa elimu ya mifano ya ufugaji kuku wa
kienyeji, kilimo na ujenzi,” alisema.
Aidha, Mwenyekiti huyo alimweleza Rais Magufuli kuwa
wamepokea vifaa vya Sayansi kutoka Marekani vyenye thamani ya Sh milioni 250
ambavyo vinatumika kwa ajili ya uboreshaji elimu chuoni hapo, ambapo pia chuo
hicho kinashiriki Maonesho
ya 77 na 88 ya TCU hivyo kuna mwamko mkubwa.
Alisema chuo kilipoanza kilidahili wanafunzi 796, hivi
sasa wana uwezo wa kudahili wanachuo wengi zaidi na sasa wamefikia 103,000.
"Kuna changamoto kubwa ya hii barabara, tunaiomba Serikali
iijenge kwa kiwango cha lami, kwani inaelekea Soga Stesheni, ikijengwa kwa lami
itasaidia kwa kiwango kikubwa katika uboreshaji huduma chuoni na wananchi kwa
ujumla, ikizingatiwa soga kuna stesheni ya reli," alisema Mwenyekiti huyo.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria, Profesa Elifas Bisanda
alisema chuo kinaunga mkono kwa dhati juhudi za Serikali huku wakimwomba asikatishwe
tamaa na baadhi ya maneno ya watu wachache.
Naye Waziri Profesa Ndalichako alimhakikishia Rais kuwa
wizara yake itaendelea kusimama kidete kuhakikisha vyuo vyote vinatoa elimu
bora kwa wanafunzi wenye sifa stahiki na si vinginevyo.
"Tutahakikisha kuna ubora wa vyuo, waendesha vyuo
hivyo na wanafunzi wenye sifa stahiki katika elimu husika na hii hata kwa chuo ambacho
kinatoa mwanafunzi anayedahiliwa pia ni sifa kwa chuo husika hivyo suala hilo
nitalitilia mkazo," alisema Waziri Ndalichako.
0 comments:
Post a Comment