Hussein Makame, NEC
Mary Longway |
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imewataka
walimu na wanafunzi nchini kuwa mabalozi wa kufikisha elimu ya mpigakura kwa
jamii inayowazunguka.
Wito huo umetolewa na Kamishna wa NEC,
Jaji mstaafu Mary Longway wakati tume hiyo ilipokuwa ikitoa Elimu ya Mpigakura
katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songea mkoani Ruvuma, ikilenga kuwawezesha
wananchi na wadau wa uchaguzi kufahamu taratibu na hatua zote za uchaguzi hadi
kutangazwa kwa matokeo.
“Binafsi nategemea kila mmoja wenu
ataweza kumuelimisha mwenzake ambaye hakupata nafasi kama hii ya kujua ni nini
elimu ya mpiga kura,” alisema Jaji Longway.
Alisema Elimu ya Mpigakura ikitolewa humwezesha
mwanafunzi kupigakura na mgombea mtarajiwa kufahamu sifa za kuandikishwa kuwa
mpiga kura au mgombea.
Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa NEC,
Emmanuel Kawishe alisema Kifungu cha 61 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kinamruhusu
mtu kupiga kura kwenye kituo alichojiandikisha na kwamba utaratibu huo huepuka
baadhi ya sehemu kuwa na wapiga kura wengi kuzidi uwezo wakati vituo vingine vikikosa
kabisa wapiga kura.
Akijibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa
na baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo, Kawishe alizungumzia elimu ya mpiga kura
kwa baadhi ya jamii zinazoishi maisha ya kuhamahama sehemu tofauti.
Alisema Tume inawajali wananchi
wanaoishi kwa kuhamahama na inawafikia wananchi hao kupitia ushirikishwaji wa
asasi za kiraia zinazokwenda kutoa elimu katika maeneo ya jamii hizo ili
kuwafikia wananchi ambao ni ngumu kuwafikia.
“Wakati mwingine ili kuyafikia makundi
hayo ya wananchi Tume inatumia ngoma na vikundi vya kiutamaduni kwenye maeneo
husika, tunatumia redio za jamii za maeneo yale, kwa hiyo asipopata elimu kwa
njia hii ataipata kupitia redio na njia za kitamaduni” alisema Bw. Kawishe.
Baadhi ya wanafunzi walizungumzia Elimu
hiyo walisema wameridhishwa na Elimu waliyoipata na imewasaidia kufahamu mambo
mengi yanayohusu Uchaguzi.
“Kwa kweli sisi wanafunzi wa Songea
Girls tumefurahishwa sana kwa kupata elimu ya mpiga kura kwa kuwa imetusaiodia
kujua haki zetu kama Watanzania hasa katika masuala ya uchaguzi” alisema
mwanafunzi Faraja Samwel Sanga.
Kwa upande wake Husna Banda alisema
amefurahi kupata elimu kuhusu kupiga kura na pia amejua umuhimu wa kupiga kura
kumchagua kiongozi ambaye anampenda kwa ajili ya maedeleo ya taifa lake.
Akitoa neno la shukrani, Mkuu wa Shule
hiyo Tupoke Ngwala alisema wanashukuru kwa nafasi ambayo wameipata ya kupata
elimu ya mpiga kura na kwamba anaamini itakuwa msaada mkubwa kwa maendeleo ya nchi
na kuahidi kuifanyia kazi kwa kadri ya uwezo wao ili kufikia lengo
lililokusudiwa.
0 comments:
Post a Comment