BAADHI ya wabunge na wasomi wameunga
mkono hatua ya Serikali kupiga marufuku matumizi ya majoho kwenye mahafali ya
ngazi za chini za elimu na kueleza kuwa itarudisha nidhamu ya elimu.
Wakizungumza na JAMBO LEO kwa nyakati
tofauti baadhi yao walisema suala hilo kwa kiasi kikubwa lilikuwa limefikia
pabaya hali iliyosababisha vazi hilo kuonekana la kawaida tofauti na ilivyokuwa
awali.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Dk Benson Bana alisema anaunga mkono hatua hiyo, kwa kuwa kila tasnia
ina heshima zake na kwamba ni kama Jeshi hivyo si kila mtu anaweza kuvaa sare
bila kigezo.
Alisema ipo haja ya kuheshimiwa kwa
utamaduni, maana si kila mtu anavaa nyota, wala sare kama urembo bali lazima
taratibu zifuatwe huku akihoji kuwa ni kwa nini suala hilo litokee nchini tu
badala ya nchi nyingine.
“Hatuwezi kusema kila mtu atavaa gauni
la harusi wakati si bibi harusi, hivyo wala haiwezekani vazi lile likavaliwa
kwenye msiba au mahali pengine isipokuwa sehemu husika, ipo haja kwa vazi hilo
lenye miiko na taratibu kuvaliwa linapotakiwa, maana kwa sasa unakuta hata
mtoto wa chekechea au darasa la saba anavaa bila sababu za msingi,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Juma Ngasongwa alisema joho ni kwa ajili ya watu waliosoma elimu fulani
ya juu, kwa kuwa ni vazi la kuheshimika na si linavyotumika sasa hali
inayosababisha kupoteza thamani yake.
Aliipongeza Serikali kwa hatua
iliyofanya ili kuwe na kiwango cha kufanana watu wanapohitimu na kuvaa majoho
hayo na si kama ilivyo sasa kila mtu anavaa bila sababu za msingi.
Mhadhiri wa UDSM, ambaye ni mtaalamu wa
masuala ya lugha, Profesa Aldin Mutembei alisema Serikali imefanya vizuri kwa
kuwa vazi hilo lilikuwa halivaliwi katika shule za msingi wala sekondari, bali
ngazi za juu zenye sifa.
Alisema endapo vazi hilo litaendelea
kuvaliwa kama ilivyo sasa, litaondoa tamaa ya watu kuendelea mbele kielimu, kwa
kuwa linaonekana halina maana hadi mwanafunzi wa chekechea anavaa bila kujua
maana yake.
Mbunge wa Ulyankulu, Joseph Kakunda
alisema ili kuweka heshima inayostahili wanafunzi wavae joho wanapomaliza
shahada zao kuanzia ya kwanza. Hiyo itasaidia kuwatia hamu walio katika ngazi
za chini za elimu wajitahidi wafikie Chuo Kikuu.
Mbunge wa Songwe, Philipo Mlugo alisema
anaunga mkono Serikali kusitisha uvaaji majoho kwa ngazi ya chini ya elimu kwa
kuwa heshima ya wahitimu ilipotea kabisa.
“Zamani ukiona picha ya mtu kavaa joho
na kofia yenye kamba unajua huyu kasoma hadi chuo kikuu, lakini leo huwezi
kujua huyu aliyevaa joho ana shahada au kidato cha nne au ni stashahada.
“Sasa hivi hata chekechea wanavaa
majoho. Nadhani kuanzia mwakani wahitimu wa ngazi mbalimbali wasiruhusiwe kuvaa
majoho zaidi ya wanachuo wanaomaliza shahada zao na kuendelea”.
Mbunge wa Igalula, Musa Ntimizi alisema
elimu ya chuo kikuu kupata shahada ni heshima kubwa zaidi katika ngazi hizo ni
vema ikaheshimiwa na kuonesha upekee.
“Tunaheshimu ngazi nyingine za elimu za
chini ila hii ni ya heshima zaidi tusiiache isifananishwe na za chini, mtoto
asione tofauti ya kidato cha nne na chuo kikuu, joho liachwe chuo kikuu
lioneshe heshima utofauti,” alisema.
Mwishoni mwa wiki, Waziri wa Elimu,
Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alipiga marufuku
matumizi ya majoho kwenye sherehe za mahafali ya ngazi za chini za elimu na
kutaka litumike kuanzia ngazi ya Shahada ili kulipa heshima vazi hilo.
Waziri Ndalichako alitoa kauli hiyo
Mbeya wakati alipokuwa anawatunuku vyeti wahitimu wa mafunzo ya uongozi na
usimamizi wa elimu kwa njia ya masafa, iliyotolewa na Wakala wa Usimamizi na Uongozi
wa Elimu Nchini (Adem).
0 comments:
Post a Comment