Suleiman Msuya
WAHITIMU wa vyuo nchini wameaswa kujiandaa kukabiliana na
changamoto za maisha mitaani kwa kujiajiri na kuachana na dhana ya kuajiriwa.
Hayo yalisemwa jana na mtoa mada katika Baraza la
Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Humphrey
Sambo wakati akiwasilisha mada iliyobeba jina la Mchango wa Chuo hicho katika
ujenzi wa maendeleo ya Taifa.
Sambo alisema ipo dhana ya wahitimu wa vyuo ikiwamo MNMA
kujiandaa kuajiriwa na kuacha kutumia taaluma zao kujiajiri.
Alisema elimu waliyopewa wanapaswa kuitumia kikamilifu
ili kusaidia jamii ili mchango wa chuo uonekane nchini.
Mtoa mada huyo ambaye pia ni Diwani wa Mbezi na mhitimu
wa chuo hicho, alisema amefanikiwa kwa kutumia elimu aliyoipata MNMA.
"Mimi nashangaa sana, mtu anamaliza chuo ana kazi ya
kutembea na cheti kutafuta kazi, mbaya zaidi umesoma MNMA, fanya ujasiriamali
achana na dhana ya kuajiriwa," alisema.
Alisema mafanikio yoyote katika maisha yanahitaji
uthubutu, jambo ambalo linashinda wasomi wengi na kubaki kufanya kazi za
kujipendekeza ili wapewe uteuzi.
Aidha, alitaka wahitimu hao kuwa mabalozi wazuri wa chuo
chao waendako na kuachana na tabia ya kulalamika na kuchafua chuo.
Mtoa mada mwingine, Renard Wigira alitaka wahitimu
kutambua jukumu lao kwa jamii kuwa ni kusaidia kila sekta.
Katibu wa Baraza hilo, John Muruga alitaka chuo kuongeza
miundombinu ili kukabiliana na wingi wa wanaodahiliwa kila mwaka.
Muruga alisema takwimu zinaonesha udahili umeongezeka kwa
asilimia 50 hivyo litakuwa jambo la ajabu kubaki na miundombinu ile ile.
"Wakati sisi tunasoma wanafunzi hawakuzidi 3,000 ila
sasa nasikia mwaka huu mmedahili 2,363 ni hatua kubwa na tutaendelea
kukitangaza chuo," alisema.
Awali akifungua Baraza hilo, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa
Shadrack Mwakalila alisema wanakabiliana na changamoto zilizopo kwa awamu na kutaka
wahitimu kuwa mfano sahihi waendako.
Mwakalila alisema wamedhamiria kukirejesha chuo katika
lengo lake la awali la kutoa wahitimu viongozi ambao watachangia maendeleo ya
nchi.
"Tumedhamiria kuwa chuo bora chenye kutoa viongozi
wasio mafisadi, wala rushwa na wasiopenda kufuata maadili kwani hilo ndilo
lengo," alisema.
0 comments:
Post a Comment