Francis Godwin, Iringa
Rais John Magufuli |
UONGOZI
wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) umempongeza Rais John Magufuli na
Serikali yake ya Awamu ya Tano kwa
jitihada anazozifanywa katika uhakiki wa watumishi
hewa na wenye vyeti bandia, kikieleza kuwa hatua hiyo ni
nzuri na itasaidia kupata
wataalamu wenye sifa.
Mwenyekiti wa
Bodi ya UoI, Askofu Dk. Odenburg Mdegela wa Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, alitoa pondezi
hizo akisema zoezi hilo linapembua mchele na chuya na kuwaacha wenye vyeti halali
pekee.
“Si sahihi mtu mmoja
akae darasani miaka mitatu na mwingine apate cheti kutoka Kariakoo tena kikiwa na
ufaulu wa juu kuliko yule aliyekaa darasani,” alisema Askofu Mdegela.
Alisema watu hao
wanapokutana kazini yule aliyepata vyeti bandia vyenye ufaulu wa juu anakuwa
hajui kazi jambo lililokuwa likirudisha nyuma maendeleo ya taasisi nyingi na Taifa
kwa jumla.
“Uhakiki wa
vyeti unapaswa kuungwa mkono na wadau wote wakiwemo wa elimu kwa kuwa hali
ilikuwa mbaya, huku wale wenye vyeti bandia vikiwa na ufaulu wa hali ya juu
ilhali hawajui kazi,” alisema Mdegela
Alisema chuo
hicho kinajipanga kuachana na mtazamo uliojengeka kwa muda mrefu wa kujiendesha
kwa kutegemea wafadhili mbalimbali wa ndani na nje ya nchi pamoja na mikopo ya
ada za wanafunzi kutoka serikalini.
Alisema
wanatarajia kuanzisha asasi itakayokuwa imeunganishwa na chuo itakayotoa mikopo
kwa ajili ya wanafunzi wanaokwama kupata huduma hiyo kutoka maeneo mengine.
Mkuu wa chuo hicho, Jaji Mkuu mstaafu Augustine Ramadhani alisema ni vema wahitimu wakawa wazalendo kwa nchi yao na kuitumia elimu waliyoipata kwa maendeleo ya watanzania wote.
Makamu Mkuu wa UoI,
Profesa Joseph Madumula alisema mazingira ya utoaji wa elimu kwa sasa yamekuwa
na ushindani mkubwa tofauti na miaka ya nyuma ambapo kulikuwa na chuo kikuu
kimoja cha Dar es Salaam kikiwa na matawi mawili ya Sokoine na Muhimbili.
Aliongeza kuwa
kwa sasa kuna zaidi ya vyuo vikuu 60 vya binafsi na serikali lakini idadi ya
wanafunzi wanaodahiliwa haijaongezeka kulingana na vyuo idadi ya vyuo.
Alisema
wamejipanga kutoa elimu shirikishi ya ujasiliamali kwa wanafunzi wote wa Chuo
hicho ili wakimaliza wasitegemee kuajiriwa tu bali wawe na uwezo wa kujiajiri
na kuzalisha ajira kwa vijana wengine.
0 comments:
Post a Comment