Grace Gurisha
Tundu Lissu |
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeshangazwa
na upande wa mashitaka kushindwa kumkamata Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu
Lissu (Chadema) licha ya kutoa hati ya kukamatwa kwa kiongozi huyo, na kusema uliogopa
kutekeleza agizo hilo halali.
Mahakama hiyo imeweka bayana kuwa haimwogopi Lissu, wala
haina mpango wa kupambana naye, bali Mbunge huyo anachotakiwa ni kufuata mfumo
wa sheria uliopo na kwa hadhi yake hatakiwi kufanya vitendo anavyofanya sasa
dhidi ya Mahakama kwa sababu yeye ni kioo cha jamii.
Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Thomas Simba
alifikia hatua hiyo jana, baada ya Lissu kuvunja masharti ya dhamana mara mbili
mfululizo katika kesi ya uchochezi inayomkabili yeye na wenzake watatu, akiwamo
Mhariri wa Gazeti la Mawio, Simon Mkina.
Simba alimhoji Wakili wa Serikali Mwandamizi, Peter Mwita:
“Amri ya kumkamata Lissu ilitolewa na wewe ulisaini hati hiyo, iweje
hakukamatwa hadi leo (jana) na wakili wake, Peter Kibatala anadai kuwa mteja
wake amekuja mwenyewe mahakamani wakati ilitakiwa aje chini ya ulinzi?”
Aliongeza: “Wewe kama wakili ulifanya jukumu gani la kuhakikisha
Lissu anakamatwa? Kwa nini hamkumkamata, hamwoni kama mnaidharau Mahakama au
mnamwogopa? …Haiwezekani Mahakama inatoa hati nyie hamuitekelezi.
“Si kwamba nataka kupambana na wewe (Lissu), hapana bali
kutokana na nafasi yako, haifai kufanya mambo kama haya. Nakwambia hatukuogopi,
tutaogopana katika mambo mengine, lakini si katika suala la kufuata sheria na wewe
ni mwanasheria unajua taratibu zote.
“Tunafanya hivi ili jamii ione, kwa sababu haiwezekani
watu wengine wanafuata utaratibu halafu wengine hawafuati, hilo
halitawezekana,” alisema Simba.
Akijibu hoja za Hakimu Simba, Wakili Mwita alisema alipeleka
hati hiyo katika kituo cha Polisi husika, hivyo hana jukumu la kumkamata.
“Lakini naomba radhi kwa kutokamatwa kwa mshitakiwa huyo na
ninaiachia Mahakama jukumu la kufuta dhamana,” alisema Mwita.
Hata hivyo, hakimu huyo alisikitika kutumia muda mwingi
kulumbana na mambo anayoyasababisha Lissu, akisema muda aliopoteza angeweza
kusikiliza shahidi hata mmoja na kumtaka Mbunge huyo kujirekebisha.
Lissu alipopewa nafasi ya kujieleza kwa nini hakuonekana
mahakamani mara mbili mfululizo bila taarifa, alidai kuwa alipata safari ya
ghafla kwenda Ujerumani na mara ya pili alishindwa kufika kwa sababu alikwenda
Mwanza kwenye kesi ya uchaguzi, ambayo ilitakiwa kwisha ndani ya muda na safari
zote hizo aliipa taarifa Mahakama kwa maandishi.
Hakimu Simba alipinga sababu hizo na kusema bado alikuwa na
nafasi ya kuandika barua na aliyodai kuandika haipo mahakamani.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Desemba 20 itakapotajwa huku Hakimu
Simba akiamuru dhamana za washitakiwa kuendelea kwa sababu upande wa mashitaka
uliogopa kumkamata Lissu.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ambao ni Mmiliki wa
Mawio Mkina, Mhariri Jabir Idrisa na Mchapaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail
Mehboob.
Ilidaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, Dar es Salaam, washitakiwa
Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi
zenye kichwa cha habari kisemacho: ‘Machafuko yaja Zanzibar’.
0 comments:
Post a Comment