Celina Mathew
Dk Philip Mpango |
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ameipa
changamoto tano Bodi ya Shirika la Bima la Taifa (NIC), akiitaka kuhakikisha
inapitia upya sheria, taratibu za kiutawala na masuala ya fedha, ili kuongeza
ufanisi na weledi kiutendaji.
Akizungumza jijini hapa juzi wakati akizindua Bodi hiyo,
Dk Mpango aliagiza ifanye kazi ili kwenda sambamba na kasi ya Serikali, ambayo
ina mengi ya kufanya, ikiwamo kukusanya kwa uhakika mapato yake.
Alitaja mambo hayo kuwa ni kusambaza huduma za bima nchi
nzima, kutoa elimu kwa wananchi kuhusu bima, ushindani katika soko huria,
huduma za bima kwa wakulima, wafugaji na wavuvi pamoja na kujenga kada ya
wataalamu wazalendo wa bima.
Katika maelezo yake, Dk Mpango alisema Bodi hiyo inapaswa
kuwa na ubunifu na kusambaza huduma za bima nchi nzima, ili wananchi wenye kipato
cha kati wanufaike nazo.
Aliitaka itoe elimu kwa wananchi kuhusu bima ya kisasa
kwa kuwa wengi hawana uelewa kuhusu suala hilo na wanatarajia mifumo ya bima ya
msingi tu jambo ambalo ni changamoto.
“Hata mimi kiongozi sina bima ya maisha na hata viongozi
wengine pia hawana, unakuta mtu anamiliki nyumba na gari la thamani, lakini
hana bima ya maisha hivyo ni vema elimu ya kutosha itolewe ili watu hai wajue maana
na umuhimu wa matumizi yake,” alisema.
Aliongeza kuwa wizara yake imejipanga kuchukua hatua za
kufuatilia taasisi zote zilizo chini ya Wizara ili kuhakikisha zinajiendesha
kwa faida na nchi inafaidika na mapato yanayotokana na biashara wanazofanya.
Alisema anajua kuwa shirika lilipitia wakati mgumu miaka
ya 90 kilipoundwa kikosi kazi cha shirika ili kuboresha huduma za bima.
“Angalieni masuala ya fedha, mikakati hata mazingira ya
soko ambayo yanaweza kukwaza shirika ili mpate ufumbuzi wa matatizo yaliyo kwenye
shirika hilo,” alisema.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Laston Msongole alisema kuanzia mwezi
ujao, NIC itagawanywa maeneo mawili; ya bima ya mali na bima ya ajali na
taratibu zimekamilika.
0 comments:
Post a Comment