John Banda, Dodoma
JESHI la Polisi mkoani hapa linashikilia watu tisa kwa
tuhuma za uvunjaji nyumba na wizi, huku wakiwa na samani za ndani zinazodhaniwa
kuwa za wizi zikiwamo kompyuta mpakato, televisheni na jokofu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamanda wa
Polisi wa Mkoa, Ernest Kimola, alisema watu hao walikamatwa Novemba 26 na 27 katika
msako uliofanywa na Polisi maeneo mbalimbali ya mkoa.
Kamanda alisema kati ya watu hao wanaume ni sita na
wanawake watatu wenye umri wa kuanzia miaka 18 ambao walikutwa na televisheni
15, deki 20, redio 10, kompyuta mpakato nane, monita saba za kompyuta, CPU za
kompyuta tatu na friji moja. Huku kati yao wakituhumiwa kuwa wezi, madalali na wanunuzi wa mali za wizi.
Kimola alisema mtandao wa wahalifu hao ni mkubwa kwa kuwa
unaunganisha sehemu za masoko ya Morogoro, Dar es Salaam na Mtwara na msako huo
unaendelea katika maeneo hayo yote ili kutokomeza mtandao huo.
Alitaja mbinu zinazotumiwa na wahalifu hao kuwa ni kuvunja
nyumba usiku au mchana wanapojiridhisha kuwa wenye nyumba hawapo karibu huku
wakitumia spana, tindo na mitaimbo kubomoa na kuvunja makufuri.
Aidha, Kamanda alitaka wananchi kujiepusha kununua mali
za wizi zinazouzwa mitaani bila risiti wakishawishika na
kuuziwa kwa bei rahisi na katika hali ya kificho na badala yake watoe taarifa Polisi
ili watu hao wakamatwe na pia wanaoiba vitu mikoa mingine na kuviuzia mkoa wa
Dodoma waache maana wataishia magerezani.
0 comments:
Post a Comment