Margareth Chambiri
MKURUGENZI wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), Kailima Ramadhani amesema jambo kubwa ambalo Watanzania wanapaswa
kujifunza kutokana na uchaguzi wa Marekani uliomalizika hivi karibuni ni
wananchi kuheshimu mifumo ya uchaguzi.
Mkurugenzi Kailima alitoa kauli hiyo kama tathimi yake
kuhusu uchaguzi wa Marekani na namna baadhi
ya watu wanavyohoji ucheleweshaji wa kutangaza matokeo ya uchaguzi unaofanywa
na Tume ikilinganishwa na ilivyofanyika Marekani.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika kipindi cha Power
Breakfast kinachorushwa na Kituo cha Redio cha Clouds FM, Kailima alisema si
sahihi kulinganisha uchaguzi wa Marekani na Tanzania, akitolea mfano wa sekta
ya mawasiliano ambayo ni muhimu katika kusafirisha vifaa na taarifa za uchaguzi
inavyokabiliwa na changamoto.
Alisema Watanzania na hasa wapiga kura wengi wanaishi vijijini
ambako baadhi ya maeneo hayafikiki kirahisi na haiwezekani Tume ikatangaza
matokeo bila kuhakikisha kuwa kila kura imehesabiwa ikiwamo ya mwananchi wa
kijijini.
Alibainisha kuwa yapo mambo ya msingi ambayo Watanzania wanapaswa
kujifunza kutokana na uchaguzi wa Marekani, kubwa ikiwa ni hatua ya kuheshimu
mifumo na mamlaka zinazosimamia uchaguzi huo.
Alitolea mfano wa uvumilivu katika kusubiri matokeo na wagombea
kuheshimu matokeo yanayotangazwa na NEC kwa mujibu wa sheria, kwani hata pale
ambapo anayeshindwa hakuridhika, anaweza kupinga matokeo kwa kufuata taratibu za
kisheria.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo alisema NEC
inakamilisha Mwongozo wa Utoaji Elimu ya Mpiga Kura wa 2015/20 ili kushirikisha
asasi za kiraia, taasisi au vikundi vya watu wanaotaka kutoa elimu hiyo.
Kwa mujibu wa Kailima, Tume imo katika hatua za mwisho za
kupitia Rasimu ya Mwongozo wa Elimu ya Mpiga Kura kwa ajili ya kuupitisha utumiwe
na wadau wa uchaguzi.
Alisema pamoja na hatua ya Tume ya kuanza kutoa elimu ya
mpiga kura mapema kuliko ilivyozoeleka na wananchi, inakusudia kupanua zaidi
wigo wa utoaji elimu hiyo kwa kushirikisha wadau wengi zaidi wakiwamo viongozi
wa dini.
Kailima alisema NEC chini ya Mwenyekiti wake Jaji mstaafu
Damian Lubuva, baadaye mwezi huu itatoa taarifa rasmi ya kuzialika taasisi na
asasi za kiraia zinazotaka kutoa elimu ya mpiga kura, kuwasilisha maombi yao ya
kibali rasmi cha kutoa elimu hiyo.
Aidha, Mkurugenzi wa Uchaguzi alitaja vigezo vya kupata
kibali cha kutoa elimu, kuwa ni pamoja na cheti cha usajili, asasi au taasisi
kufanya kazi nchini kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kuwasilisha majina
ya watendaji wa juu.
NEC imeanza utekelezaji wa utoaji elimu hiyo kwa kushiriki
maonesho mbalimbali yakiwamo ya biashara ya kimataifa na ya wakulima na
kutembelea na kutoa elimu kwenye shule kadhaa za sekondari nchini.
0 comments:
Post a Comment