Grace Gurisha
WAFUASI wa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na
Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif
Sharif Hamad wamegeuka sinema ya bure baada ya kutwangana makonde hadharani
katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.
Ugomvi huo ulioibua mapambano ya ngumi ulitokea jana baada
ya wafuasi wa Maalim Seif waliokuwa mahakamani hapo kumzuia Profesa Lipumba kuingia
kusikiliza kesi inayomkabili iliyofunguliwa na Baraza la Wadhamini wa Chama
hicho.
Profesa Lipumba alifika mahakamani hapo saa mbili
asubuhi, ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kesi hiyo dhidi yake kufunguliwa ikidai
kuwa yeye si mwanachama halali wa CUF.
Baada ya kesi za Jaji Sakiet Kihio kuitwa na mtoa
matangazo wa Mahakama kwa kuelekeza kuwa kesi za Jaji huyo zinasikilizwa chemba
watu wote waliinuka na kuelekea katika chumba hicho wakiwamo mawakili wa pande
zote.
Walipofika kwenye mlango wa chumba cha Mahakama, wafuasi
wa Maalim Seif walisimama mlangoni kumzuia Profesa Lipumba kwa madai kuwa wanaotakiwa
ni mawakili tu na si watu wengine, ndipo wafuasi wa Mwenyekiti huyo walipoingilia
kati na kuwashushia kipigo watu hao.
Hatua hiyo ilishuhudia mabadilishno ya makonde na kusababisha watu wawili upande wa
Maalim Seif kuumia, na kusababisha Jaji Kihio
kutoa amri kuwa waingie mawakili na walalamikiwa ndipo Lipumba naye akaingia.
Kesi iliendelea kusikilizwa, huku askari wakiimarisha ulinzi
wa chumba hicho, kwa sababu wakati wafuasi hao wanapigana wao hawakuwapo. Jaji
Kihio aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 6 zitakaposikilizwa sababu za Bodi
hiyo kumtaka ajitoe kusikiliza kesi hiyo.
Baada ya kesi hiyo kuahirishwa, Profesa Lipumba alitolewa
na wafuasi wake akiwa chini ya ulinzi mkali kwa kuhakikisha kuwa hakuna mtu
atakayemgusa na alipofika nje, alipokewa na wafuasi wengine wakiwa na mabango
yenye ujumbe dhidi ya Maalim Seif.
Bango moja liliandikwa: ‘Maalim Seif kama ulikaa na CCM
umeshindwaje kukaa na Mwenyekiti wako Lipumba mkayamaliza’, linguine: ‘Maalim
Seif tulijua CCM ndiyo kiboko yako, kumbe Lipumba ndiye mwamba wako’, huku
wakiendelea kuimba wimbo wa chama hicho.
Lipumba alipoingia kwenye gari alishusha kioo na kusalimu
wafuasi wake kwa kuwapungia mikono, huku wengine wakisukuma gari lake kabla ya kuondoka
eneo la Mahakama.
Hata hivyo, Profesa Lipumba hakutaka kuzungumza chochote,
akitumia muda wake mwingi kutabasamu na kupunga mkono. Wakati hayo yote yakifanyika,
nje ya Mahakama askari walikuwa tayari wametenga makundi hayo mawili, lakini
bila kufanya hivyo, watu hao wangeendelea kupigana.
Wakili wa Bodi hiyo, Juma Nassoro akiwa nje ya Mahakama, alimkariri
Jaji akisema Desemba 6 kesi hiyo ataisikilizia kwenye Mahakama ya Wazi, kwa
sababu alikuwa hajui kama watu ni wengi, kwa hiyo hataifanyia tena chemba.
Pia alisema Profesa Lipumba, Msajili wa Vyama vya Siasa,
Jaji Francis Mutungi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na wafuasi 11
wamewasilisha pingamizi mahakamani hapo, kuwa wateja wake walifungua kesi hiyo
bila idhini ya Mahakama na pia Maalim Seif alibariki kufunguliwa kwa kesi hiyo
bila idhini ya Bodi.
Baadaye mawakili wa CUF, Nassor na Hashimu Mziray waliwasilisha
ombi la kumtaka Jaji Kihiyo ajitoe kusikiliza shauri hilo kwenye Mahakama hiyo,
na sababu za kumkataa zitaelezwa Desemba 6 saa saba mchana wakati kesi hiyo
itakapokuja kusikilizwa.
Walalamikaji hao wanaomba Mahakama itengue barua ya Msajili
ya kumtambua Profesa Lipumba kuwa mwanachama hai wa CUF. Wakili Mziray alisema walifungua kesi hiyo kwa
hati ya dharura kutokana na mambo yalivyo sasa ndani ya chama hicho, kwa sababu
hawajui hata ofisi zingine zinaendeshwaje.
Alisema katika maombi hayo, wanaiomba Mahakama mambo
matatu, ambayo ndiyo yanasababisha kufukuta kwa mgogoro, kwa hiyo wanaomba
yatenguliwe ili shughuli za kisiasa ziendelee.
Alisema mambo hayo ni pamoja na Mahakama kutengua barua
ya Msajili ya Septemba 23 ambayo ilitengua uamuzi wa CUF wa kumfukuza uanachama
Profesa Lipumba na kumhalalisha kuwa mwanachama hai wa chama kama Mwenyekiti.
0 comments:
Post a Comment