*Azungumzia mafanikio yake ya mwaka Ikulu
*Ataka wananchi wamuunge mkono kwa dhati
Fidelis Butahe
Ali Hassan Mwinyi |
RAIS mstaafu Ali Hassan Mwinyi
amempongeza Rais John Magufuli kwa mafanikio aliyopata katika mwaka mmoja
madarakani hasa kwa kupambana na rushwa.
Ameifananisha kasi yake ya kupambana na
rushwa na dhoruba ya mawimbi ya tsunami yaliyokumba nchi kadhaa duniani miaka
12 iliyopita.
Hii ni mara ya kwanza kwa Rais mstaafu
Mwinyi kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli Ikulu Dar es Salaam, tangu
kuanza kwa awamu ya tano ya uongozi wake.
"Rushwa ilikuwepo tangu enzi za
Nyerere (Mwalimu Julius), aliipondaponda kabisa, lakini hakuimaliza, na sote
tuliosalia ni hivyo hivyo, kila mmoja amefanya kwa kiasi chake, lakini Rais
Magufuli kwa mwaka mmoja ameleta tsunami, nafurahi sana," alisema Mwinyi
jana baada ya kukutana na Rais Magufuli Ikulu, Dar es Salaam.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya
Rais Ikulu, Gerson Msigwa iliyotolewa jana ilisema baada ya mazungumzo hayo,
Mwinyi alisema lengo la kukutana na Rais Magufuli na kuzungumza naye kwa mara
ya kwanza, ni kumpongeza kwa kutimiza mwaka mmoja madarakani na kazi kubwa
aliyofanya katika kipindi kifupi cha uongozi wake.
Alizungumzia Mahakama ya Mafisadi kama
moja ya mafanikio yake akisema imekuwa kwenye Ilani ya CCM tangu mwaka 2010,
lakini ilizungumzwa zaidi kwenye uchaguzi uliopita na Magufuli akaibeba kwenye
kampeni zake, wakati Taifa likipigia kelele ufisadi uliokithiri nchini.
Katika kampeni hizo Rais huyo wa Awamu
ya Tano aliahidi kuanzisha Mahakama hiyo kwa lengo la kuhakikisha kesi za aina
hiyo zinakuwa na Mahakama yake, kusikilizwa kwa muda mfupi na wahusika
kuchukuliwa hatua stahiki.
Baada ya kuapishwa kuwa Rais Novemba 5,
Dk Magufuli amepambana na rushwa na ufisadi ikiwa ni pamoja na ‘kutumbua’
baadhi ya watendaji wa Serikali wanaotajwa kwa tuhuma za kutafuna fedha za
umma.
Wakati akihutubia Bunge Novemba mwaka
jana mara baada ya kuapishwa, Rais Magufuli aliahidi kuanzishwa kwa Mahakama
hiyo ambapo Januari alimtaka Jaji Mkuu, Othman Chande kutosubiri Bunge
kupitisha Sheria ya Uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi, badala yake waanze
maandalizi ya kuiendesha Mahakama hiyo.
Aprili akiwa bungeni, Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa alisema Mahakama ya Rushwa ambayo iliahidiwa na Rais Magufuli wakati
wa uchaguzi uliopita, itaanza kufanya kazi hivi karibuni kwa kushughulikia kesi
10 kubwa ambazo uchunguzi wao umekamilika.
Katika mazungumzo hayo, Rais Mwinyi
alisema baadhi ya maeneo ambayo Dk Magufuli ameyafanya kwa mafanikio makubwa ni
mapambano dhidi ya rushwa na kubainisha kuwa hatua zilizochukuliwa katika
kipindi hicho zimedhihirisha kasi kubwa ya kukabiliana na tatizo hilo
ikilinganishwa na wakati uliopita.
Alisema eneo lingine ni kuimarisha
utendaji kazi serikalini na kwamba hatua zilizochukuliwa na kiongozi huyo wa
nchi ziliongeza kasi zaidi huku akitoa mwito kwa viongozi na wananchi kumuunga
mkono.
"Tuliobaki tumsaidie, tumsaidie kwa
kumwombea dua, tumsaidie kurekebisha kwa kusema ukweli pale ambapo watu
wanapotosha, tuseme,” alisema.
“Tusiwaache watu wakapata nafasi ya kusema
uongo, kila mtu anaweza kuwa anasema kutokana na nia yake na lengo lake, lakini
hakuna asiyejua kuwa kazi aliyofanya mwenzetu ni nzuri, nzuri, nzuri ya ajabu,”
aliongeza.
Katika mwaka wa fedha wa 2016/17
Serikali ilieleza kuwa itaendelea kuchunguza tuhuma 3,444 zilizopo na mpya
zitakazojitokeza na kukamilisha uchunguzi wa tuhuma 10 za rushwa kubwa.
Rais Magufuli pia alikutana na kufanya
mazungumzo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.
0 comments:
Post a Comment