Sharifa Marira
Magdalena Sakaya |
YALIYOMKUTA Katibu Mkuu wa CUF mkoani
Mtwara ya kukwama kwa mikutano yake ndiyo
yatakayomkuta Mwenyekiti wa Chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, atakapokwenda
Zanzibar.
Mkutano wa Maalim Seif uliokuwa na lengo
la kukagua shughuli za chama, kupata maoni na mapendekezo kuhusu namna ya
kuboresha utendaji wa chama ngazi ya chini, ulipangwa kufanyika Novemba 19 kwenye
Chuo cha Stella Maris, Mtwara ulizuiwa na Jeshi la Polisi.
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na
Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Bara, Magdalena Sakaya alipozungumza na waandishi
wa habari kuhusu kukwama kwa ziara ya Maalim Seif, Mtwara, akidai kwamba hapana
sababu ya kusaka mchawi kwa kuwa hawakufuata taratibu.
Sakaya ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua,
alisema ni vigumu Profesa Lipumba kwenda Zanzibar kufanya mikutano ya kuimarisha
chama, kwani anatakiwa awasiliane na Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar,Nassor Mazrui,
ili amwandalie mikutano jambo ambalo haliwezekani bila kupatana viongozi hyao wawili
wanaokinzana.
‘’Kilimchomkuta Maalim Seif alistahili
na kamwe asitafute mchawi kwani mikutano ambayo alitaka kuifanya hakufuata
taratibu ikiwa ni pamoja na kunipa taarifa mimi, ili niwasiliane na makatibu wa
wilaya waandae mikutano yao na polisi walikuwa sahihi kuuzuia kwani kungetokea
fujo,’’ alisema Sakaya na kuongeza:
‘’Hata leo mimi au Profesa Lipumba
tukitaka kwenda Zanzibar lazima tuwasiliane na Mazrui hatuwezi kufika moja kwa
moja, tunaweza kukwama, hatima ya mikutano yetu kule iko mikononi mwa Maalim
Seif na Mazrui.’’
Alisema kinachotakiwa kufanyika ni
viongozi hao wawili, Maalim Seif na Profesa Lipumba kukubali kukaa meza moja
kumaliza tofauti zao na kunusuru chama.
“Maalim Seif anakubalika Zanzibar, Lipumba
Bara, hatima ya CUF ni lazima viongozi wakae chini hakuna njia nyingine,
kinachoumia ni chama, tusiweke mbele kushinda na kushindwa,’’ alisema Sakaya.
Alisema watu wamezoea kuzusha maneno,
kwamba polisi wanaruhusu mikutano ya Lipumba na kuzuia ya Maalim Seif, lakini
kilichotokea Mtwara kilikuwa sahihi kwani taratibu za kuomba mikutano hazikufuatwa.
“Polisi waliona kuruhusiwa kwa mkutano
huo lolote lingeweza kutokea kwani waliokwenda kuomba kibali hawakufuata
utaratibu na si viongozi bali wanachama wa kawaida, ambao hawana nafasi ya
kuomba kibali chochote, ndiyo maana polisi walitutaka kama chama tukae
tuelewane ndipo tuombe kibali,” alisema.
Alisema kilichotokea Mtwara ni sehemu tu
ya kinachoweza kutokea maeneo mengine Bara, endapo Maalim Seif ataendelea na utaratibu
wa kukiuka Katiba na taratibu halali za chama na kwamba yuko tayari kumwandalia
mikutano, ila isiwe ya kunadi chuki au kumkataa Profesa Lipumba.
Sakaya aliwahadharisha wanasiasa wanaoingilia
mgogoro huo kwa lengo la kubomoa chama kwamba wakae mbali, hawahitaji msaada wa
kichochezi.
“Kuna wanasiasa wanataka kutumia mgogoro
huu kuendeleza vyama vyao, wakae chonjo, hakuna chama ambacho hakijapata
kukumbwa na migogoro, lakini CUF hatujawahi kuviingilia kwa nia ya kuvibomoa
wala kujinadi kwa ajili ya chama kingine,” alionya Sakaya.
0 comments:
Post a Comment