Jemah Makamba
MTU ambaye hakufahamika jina mara moja,
amezua mtafaruku kwenye viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Ilala baada ya
kutembea kwa magoti akiomba radhi watu watatu tofauti, kabla ya kukimbia baada
ya kushangilia Said Mrisho kutobolewa macho na Scorpion mbele ya wazazi wake
bila kujua.
Tukio hilo la aina yake lilitokea jana muda
mfupi baada ya Scorpion kufikishwa mahakamani hapo, ambapo mtu huyo bila kujua
alijikuta katikati ya mama mzazi wa Mrisho, mjomba wake na dada yake na kutoa maneno ya kashfa akishangilia kitendo
hicho.
Ndugu hao waliofika hapo kufuatilia kesi
dhidi ya mtuhumiwa wa Mrisho, wakiwa wamesimama nje ya Mahakama na bila kujua
uhusiano walionao na mlalamikaji, walishangaa kusikia mtu huyo akimwaga tuhuma dhidi
ya Mrisho na kudai alistahili adhabu hiyo.
JAMBO LEO lililokuwa eneo la tukio,
lilimsikia akidai kuwa Mrisho ana tabia mbaya hivyo ni haki yake kutobolewa
macho kwani pia ni ‘kibaka’ aliye na kikundi chake wanaofanya uharifu na hivyo
Scorpion amemkomesha.
Maneno hayo yaliamsha hasira za Mama Mrisho,
aliyekuja juu na kueleza kuwa yeye ndiye mzazi wa kijana aliyetobolewa macho,
huku ndugu wengine wakimshika mtu huyo kwa hasira.
Tukio hilo lilimfanya kupiga magoti huku
akitetemeka na kwenda kwa mmoja mmoja kumwomba radhi.
Mtu huyo alitembea kwa magoti kwenda kwa
mama wa Mrisho, kisha kwa dada yake na kumalizia kwa mjomba mtu, huku machozi
yakimlengalenga.
"Ndugu zangu Waislamu wenzangu,
mimi ni mtu mzima nina miaka 46, naombeni mnisamehe sana, sijui chochote. Haya
maneno nimeyasikia tu huko mtaani, lakini simjui Scorpion na hata sijawahi
kumwona, naombeni msamaha sana," alisema mtu huyo.
Alijieleza kuwa alifika mahakamani hapo
kufuatilia kesi ya mirathi akisubiri kuitwa, lakini akisamahewa hatakaa eneo
hilo tena bali ataondoka na hatasikiliza kesi yake.
Akiwa amepiga magoti, mjomba wa Mrisho
alimwambia asimame na aondoke mbele yao, aliinuka na kutimua mbio kuelekea nje
ya lango la kuingilia mahakamani hapo
bila kugeuka na kutokomea.
Katika hatua nyingine, siku 28 zimetosha
kwa Polisi kukamilisha upelelezi wa kesi
dhidi ya Salum Njwete au ‘Scorpion’ tangu alipofutiwa mashitaka ya awali na
kufunguliwa upya ambapo atasomewa maelezo ya awali Novemba 30.
Kukamilika kwa upelelezi huo, kunaweza
kutafsiriwa kuwa ni mabadiliko katika kitengo hicho chenye malalamiko mengi ya
kuchukua muda mrefu kukamilisha upelelezi wa kesi.
Scorpion anashitakiwa kwa madai ya
kumwibia Saidi Mrisho vitu na fedha zikiwa na thamani ya Sh 476,000 na kabla na
baada ya kumwibia alimjeruhi kwa kumchoma kisu tumboni, mabegani na kumtoboa
macho maeneo ya Buguruni Sheli Septemba
tisa.
Kutokana na tuhuma zinazomkabili hawezi
kupata dhamana hivyo ataendelea kukaa mahabusu.
Scorpion alifikishwa mahakamani kwa mara
ya kwanza Oktoba 19 na alifutiwa mashitaka la mara ya kwanza kabla ya
kushitakiwa upya.
Jana, mshtakiwa huyo alifikishwa kwa
mara ya tatu, baada ya siku 14 kupita ambapo Mahakama ilielezwa upelelezi wa
kesi yake umekamilika.
Hakimu Haule alihairisha kesi hiyo hadi
Novemba 30 itakapotajwa kwa ajili ya mtuhumiwa kusomewa maelezo ya awali na
kuanza kusikilizwa.
0 comments:
Post a Comment