Mwandishi Wetu
MABORESHO ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na
uchumi wa kati itafanikiwa ikiwa Serikali itaboresha sera za sekta hiyo na
kuweka mazingira yanayovutia uwekezaji kwa wazawa na wageni.
Tangu aingie madarakani, Novemba 5 mwaka jana, Rais John
Magufuli amekuwa akihimiza kubuniwa na kutekelezwa kwa mipango ya kujengwa
viwanda ili pamoja na mambo mengine, vichangie kuongeza thamani ya mazao ya
kilimo.
Katibu Mtendaji wa shirika lisilo la Serikali la Wadau wa
Kilimo (Ansaf), Audax Rukonge amesema azma hiyo inapaswa kutekelezwa kwa kutoa
kipaumbele kwa viwanda vidogo visivyohitaji mitaji mikubwa, vikitoa ajira
nyingi na kuwa karibu na wananchi wa ngazi za chini kwenye jamii.
Rukonge alisema hayo jana ofisini kwake Dar es Salaam,
wakati akitoa taarifa ya kongamano la wadau wa kilimo litakalofanyika Dodoma
Desemba mosi na 2, likijielekeza katika nafasi ya kilimo kwenye viwanda.
“Hatutaipeleka nchi kwenye ushindani wa viwanda ikiwa
mkakati wetu hautaiwezesha sekta ya viwanda vidogo kushamiri, ili kuzalisha
bidhaa zitakazochatuliwa na viwanda vya kati kabla ya kufikia vikubwa,”
alisema.
Pamoja na maboresho ya viwanda, Rukonge alisema uboreshaji
wa miundombinu na sera yanapaswa kutoa jawabu la kulinda mazao yanayozalishwa
nchini bila kuathiri taratibu za Shirika la Biashara la Kimataifa (WTO).
Alisema nchi kadhaa duniani zinatekeleza mahitaji ya kisera
kulinda bidhaa za ndani zikiwamo za kilimo, kama ilivyo India inavyotoza
asilimia tano kwa korosho inayoingizwa kutoka nje ya nchi hiyo.
“Hivi sasa uzalishaji wa korosho India umeongezeka kwa kiasi
kikubwa hivyo kuifanya nchi hiyo kutoza asilimia tano ya thamani ya korosho
inayoingizwa kutoka nje ikiwa katika hali ghafi, ili kulinda korosho wanayozalisha,”
alisema.
Pia Rukonge alisema pamoja na kulinda uzalishaji wa ndani,
ipo haja ya kuwapo ruzuku kwa wakulima ili kukuza uzalishaji, akitoa mfano wa
Umoja wa Wabanguaji Wadogo wa Korosho nchini, asilimia 70 ya wanachama wake
wakiwa ni wanawake.
Azimio la Maputo la Mwaka 2003 lililosainiwa na wakuu wa nchi
za Afrika, lilihimiza kutengwa kwa bajeti za mataifa hayo kufikia asilimia 10,
ili kuongeza ufanisi katika sekta hiyo ambayo uchumi wake unategemewa na
takribani asilimia 80 ikihusu watu wanaoishi vijijini.
Kuhusu kongamano la Dodoma, Rukonge alisema limejielekeza
katika masuala ya kilimo kwenye viwanda, kutokana na azma ya Serikali ya awamu
ya tano kutilia mkazo mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa yenye uchumi wa
viwanda.
Kongamano hilo litajumuisha washiriki wanaokadiriwa kufikia
150 wakiwamo watafiti watakaowasilisha matokeo ya utafiti wao kuhusu sekta za
kilimo na kiwanda.
0 comments:
Post a Comment